Adhabu ya kifo kufumuliwa

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 12:22 PM Apr 30 2024
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Pinda Chana.
PICHA: MWANDISHI WETU
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Pinda Chana.

SERIKALI inatarajia kufanya maboresho ya sheria mbalimbali ikiwamo ya adhabu ya kifo na kifungo cha maisha katika mwaka wa fedha 2024/25.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Pinda Chana, ameyasema hayo bungeni wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Amesema katika kipindi hicho serikali inatarajia kufanya uratibu, tathmini na maboresho ya sheria mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya mapitio ya mifumo ya sheria inayosimamia elimu na michezo ya kubahatisha.

“Katika mwaka ujao wa fedha tutafanya mapitio ya adhabu ya kifo na kifungo cha maisha sambamba na kufanya utafiti wa mfumo wa sheria unaosimamia utatuzi wa migogoro ya kibenki na taasisi za fedha,” amesema Dk. Pindi.

Wanaharakati mbalimbali nchini wanapinga kuwapo kwa adhabu ya kifo kwa madai kuwa ni ya kikatili na inayopinga haki ya msingi ya kuishi.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ni kati ya taasisi zinazopinga adhabu hiyo ambacho kimedai kuwa adhabu hiyo ikishatekelezwa haiwezi kubadilishwa hata kama kuna makosa yametokea.

LHRC inadai kuwa kuna mifano mingi katika nchi mbalimbali ulimwenguni kwa watu kunyongwa hadi kufa kwa maamuzi ya mahakama na baadaye kuthibitika kwamba hawakutenda makosa yaliyosababisha adhabu hiyo. 

Aidha, nchi nyingi duniani zimeendelea kuondoa adhabu ya kifo. Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kimataifa la Amnesty International ya mwaka 2018, jumla ya nchi 106 duniani zilikuwa zimeondoa adhabu ya kifo kwenye sheria zao kufikia Desemba 2017. 

Pia, jumla ya nchi 142 zilikuwa zimeondoa adhabu hiyo na kwa upande wa Afrika, takribani nchi 20 za Kusini mwa Jangwa la Sahara zimeondoa adhabu hiyo ikiwamo Guinea Bassau, Djibouti, Afrika Kusini, Senegal, Rwanda, Burundi, Togo, Gabon na Congo-Brazzaville.

Kwa mwaka 2017, asilimia 84 ya adhabu za kifo zilizotekelezwa, zilitekelezwa katika nchi nne pekee duniani.

Akiwasilisha makadirio ya wizara yake, Dk. Pindi  amesema pamoja na mambo mengine Wizara ya Sheria na Katiba inatarajia kutekeleza mambo 15 ambayo yapo katika vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha 2024/25 na kuomba kuidhinishiwa Sh. bilioni 441.2 ili kutekeleza kazi hiyo.

Amesema mambo mengine ni pamoja na kutunga Sera ya Taifa ya Haki Jinai, kushughulikia masuala ya kikatiba ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya Katiba na uraia kwa umma.

Amesema pia wanatarajia kusimamia mfumo wa haki na utoaji haki ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya Mahakama, kuharakisha mashauri ya kawaida na kumaliza mashauri ya muda mrefu.

Vilevile,  amesema Wizara ya Katiba na Sheria inatarajia kufanya uandishi wa sheria ikiwa ni pamoja na kuandaa toleo la sheria ndogo zilizofanyiwa urekebisho mwaka 2025 na kuimarisha marejeo na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mikataba iliyosainiwa.

Kadhalika, ametaja uendeshwaji mashtaka ya jinai, kuimarisha utenganishaji wa shughuli za mashtaka na upelelezi, kushughulikia uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi wa migogoro ya kibiashara, sheria za kimataifa na mikataba.

Amesema shughuli nyingine ni pamoja na kuimarisha usajili wa matukio muhimu ya binadamu pamoja na usajili na ufilisi katika mikoa yote ya Tanzania Bara.

Vilevile,  amesema kuratibu ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa sheria za utajiri asili na maliasilia za nchi, kushughulikia urejeshwaji wa wahalifu na masuala ya ushirikiano wa kimataifa kwenye makosa ya jinai.

Kuhusu uimarishaji matumizi ya TEHAMA katika utoaji haki na huduma za kisheria, Dk. Pindi  amesema serikali itaendelea kuboresha mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano kama nyenzo muhimu ya kuboresha utoaji wa huduma.

Pia,  amesema wataboresha utendaji na maendeleo ya rasilimali watu ya Wizara ya Katiba na Sheria na taasisi zake ikiwamo ajira, uteuzi, nidhamu na maadili.