Wadaiwa kutoroka na fedha za mauzo ya maji Shinyanga

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 07:15 PM Apr 30 2024
Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Elias Masumbuko (aliyesismama), akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha robo tatu ya mwaka.
Picha: Marco Maduhu
Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Elias Masumbuko (aliyesismama), akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha robo tatu ya mwaka.

BAADHI ya wananchi waliopewa jukumu la kusimamia vituo vya kuuzia maji (maghati) katika Halmashauri ya Manispaa Shinyanga, wadaiwa kutoweka na fedha za mauzo ya maji yaliyofanyika katika halmashauri hiyo.

Hayo yamebainisha leo Aprili 30,2024 kwenye kikao cha Baraza la madiwani la manispaa hiyo, wakati wa uchangiaji wa taarifa ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA).

Kwa mujibu wa Meya ya Manispaa ya Shinyanga, Elias Masumbuko, watu hao waliwekwa katika maghati hayo na SHUWASA wenyewe, ili awaisie katika usimamizi wa mauzo ya maji.

"SHUWASA mnapotuambia kwamba maghati hayatoi maji sababu ya madeni, tunashindwa kuwaelewa, hebu tupeni ufafanuzi mzuri kwanini maji hayatoki, sababu taarifa tulizonazo ni kwamba watu ambao mliwaweka ili wauze maji ndiyo wametoroka na fedha za mauzo, kimsingi, ni watu wenu wenyewe, sasa kwanini watu hawapati maji," amehoji Masumbuko.

Nao baadhi ya madiwani akiwamo Mariamu Nyangaka wa Kitangili, wakati wakichangia taarifa hiyo ya SHUWASA, wamehoji kwanini baadhi ya vituo vya kuchotea maji havitoi huduma hiyo kwa wananchi na kwamba vimefungwa kabisa.

Mkurugenzi wa SHUWASA, Mhandishi Yusuph Katopola, akitoa majibu kwenye baraza hilo, amekiri kwa kusema: “Maghati  ya kuchotea maji yamekuwa na changamoto ya usimamizi, kwa watu kukosa uaminifu na kutumia fedha za mauzo ya maji.” 

Amesema sababu kubwa ambayo kwayo maghati mengi yamesitisha utoaji wa huduma ya maji ni madeni, kutokana na wasimamizi wake kutolipa bili za maji, na kwamba kwa sasa wanachokifanya ni kuangalia utaratibu wa kuweka mita za malipo ya kabla.

Ametaja sababu nyingine maghati hayo kufungwa, inatoka na kwamba matumizi ya maji kwa wananchi yamekuwa madogo, kwa kuwa wengi wameishaunganisha mambomba katika nyumba zao na hivyo kutohitaji huduma hiyo kutoka katika maghati hayo.

"Watu ambao tunawaweka kusimamia mauzo ya maji hua tunawalipa asilimia 20 ya ukusanyaji wa mapato, sasa kama kwa mwezi mtu anauza maji Sh.Elfu 20 ina maana alipwe Sh.Elfu 4, kitu ambacho wengi hua hawakubali ndiyo maana uaminifu unakuwa mdogo," amesema bosi huyo wa SHUWASA.

Aidha, amewaomba madiwani kwamba kwenye maeneo ambayo maghati yanahitajika, ni vema wananchi wakawasiliana na SHUWASA, ili huduma hiyo iweze kurejeshwa, licha ya kuwapo kwa madeni hayo, sambmba na kupata watu waaminifu ambao watasimamia mauzo ya maji.

Kikao hicho cha baraza hilo limepokea na kujadili taarifa mbalimbali, zikiwamo zile za Kamati ya Kudhibiti Ukimwi, Mipango Miji na Mazingira, Uchumi Afya na Elimu, pamoja na Fedha na Utawala.