Zingatieni sheria za usalama barabarani ili mnusuru maisha ya wananchi

By Gideon Mwakanosya , Nipashe
Published at 05:32 PM Apr 30 2024
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarari Mkoa wa Ruvuma (RTO) Mrakibu msaidizi wa Polisi (ASP) Issa Milanzi
Picha: Gideon Mwakanosya
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarari Mkoa wa Ruvuma (RTO) Mrakibu msaidizi wa Polisi (ASP) Issa Milanzi

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarari Mkoa wa Ruvuma (RTO) Mrakibu msaidizi wa Polisi (ASP) Issa Milanzi ametoa onyo kwa madereva wote wanaoendesha magari mabovu ya kubebea wanafunzi wanaosoma katika shule zao.

Akizungumza na Madereva wa magari ya wanafunzi (School bus) amewataka kutumia magari yaliyo vizuri na mazima na kuacha kutumia magari mabovu kubebea wanafunzi ili kuepukana na ajali zisizo za lazima.

"Kuna baadhi ya madereva mmekuwa na kawaida ya kutumia gari mbovu kuwachukua wanafunzi kuwapeleka shuleni na kuwarudisha nyumbani kwao,hii tabia iishe mara moja na kama kuna gari mbovu peleke service, likishakaa vizuri tumieni sisi kama jeshi la polisi Kikosi cha usalama barabarani hatutawavumilia"amesisitiza RTO Milanzi.

Aidha amewataka Maedereva wa magari hayo kuongeza umakini katika majira haya ya Mvua za masika zinazoendelea kunyesha Mkoani Ruvuma ambapo  zinaweza kupelekea barabara nyingi kuaribika ili kuepuka ajali zisizo za lazima.

Sambamba na hilo amewakumbusha  madereva kuwa wameaminiwa na wazazi pamoja na wakuu wa shule katika kulinda usalama wa watoto pindi wanapowabeba wanafunzi kuwapeleka shule hivyo watumie vibali hivyo kuhakikisha wanafunzi hao wanakuwa salama.

Pia ASP Issa Milanzi amesema Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa  wa Ruvuma kimejipanga kufanya Operesheni kwa ajili ya kukamata madereva wote wanaovunja sheria  za usalama barabarani pamoja magari mabovu  na kuwafikisha mahakamani kwa hatua zaidi ikiwa pamoja na kuwafungia reseni zao.

ASP Milanzi alihitimisha kwa kutoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanakuwa karibu na watoto wao pale wanapokuwa wamerudi shule ili kujua maendeleo yao ya elimu na kuweza kugundua changamoto zinazoweza kuwakabili hususani vitendo vya ukatili ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa mapema kama vikibainika kutendeka.