SIKU chache baada ya roboti Eunice kuwa gumzo katika mitandao ya kijamii, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA nchini, Dk. Nkundwe Mwasaga, amesema lengo la kuleta roboti hiyo ni kuimarisha ubunifu wa kidigitali katika kukuza uchumi wa taifa.
Akizungumza na Nipashe Digital, Dk.Mwasaga amesema teknolojia ya roboti inaweza kusaidia katika majukumu mbalimbali ikiwamo ajali inapotokea.
"Huu ni ubunifu ambao tumeufanya kati ya Tume ya TEHAMA na wizara yetu, kwa sababu wizara yetu ndio inayosimamia mambo yote ya kidijitali kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa shindani na inakuwa katika viwango vya kidunia vya mambo hayo,” amesema.
Ameongeza: "Tumefanya mambo mengi ambayo mmeyasikia, tumepeleka mawasiliano sehemu mbalimbali ikiwamo kujenga mkongo, sasa, tunaenda katika teknolojia ibukizi katika hizo, teknolojia ambayo ina jina kubwa sana ni akili mnemba na mambo ya roboti kama mnavyoiona,” alisema.
Amebainisha kuwa tume ina mpango wa kununua maroboti mengine ambayo watakuwa wanafanya kazi na vyuo mbalimbali na watu wengine.
"Kazi kubwa ni kukuza ubunifu wa kidijitali na maroboti kama haya yana matumizi mengi ya kijamii, tulichokifanya hapa, tumemleta huyu roboti na roboti kama mnavyofahamu anaitwa Eunice na yeye amewekewa teknolojia za kisasa sana, anaweza kuona na anaweza kusikia na anaweza kufanya mazungumzo na watu,” amesema.
Amesema jukumu lao kwa sasa ni kutambua roboti zipi zitatumika maeneo ya viwandani, ni roboti zipi ambazo zinatumika katika maeneo ya super market, roboti zipi zinatumika katika maeneo ya ajali.
Ameongeza: "Lakini, ninataka kuwatoa wasiwasi watu kuhusu kupoteza kazi, siyo kweli. Roboti zitatufanya kufanya shughuli zetu kwa tija zaidi kwa mfano kama ulikuwa unafanya uzalishaji kwa wiki moja sasa hivi unaweza kufanya kwa muda mfupi zaidi”.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED