CECAFA kukutana Juba leo

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 09:12 AM Jan 22 2025
CECAFA
Picha: Mtandao
CECAFA

MKUTANO Mkuu wa mwaka wa Baraza la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), unatarajiwa kufanyika jijini Juba, Sudan Kusini leo.

Mkuu wa Idara ya Habari na Masoko wa CECAFA, Andrew Oryada, aliliambia Nipashe jana mkutano huo utahusisha Marais na Makatibu wakuu wa nchi wanachama wa baraza hilo ambao wote wameshafika Sudan Kusini kwa ajili ya kikao hicho.

"Tunatarajia marais na makatibu wakuu wote wa nchi 12 wanachama wa CECAFA kuhudhuria mkutano huu, agenda mbalimbali zitajadiliwa, kalenda za mashindano pia zitapangwa katika mkutano huu," Oryada alisema.

Naye Msemaji wa Shirikisho la Soka la Sudan Kusini (SSFA), Albino Kuek, alisema maandalizi kuelekea mkutano huo yamekamilika na wanatarajia wajumbe wa CECAFA watashuhudia miradi mbalimbali ya maendeleo ya mchezo huo nchini humo.

"Kufanyika mkutano huu hapa kutatoa ujumbe kwa dunia kuwa Sudan Kusini ina fursa mbalimbali, kwetu hii ni sehemu ya kuonesha mapinduzi ya michezo nchini kwetu, " alisema Kuek.

CECAFA inaundwa na nchi 12 ambazo ni Tanzania Bara, Tanzania Visiwani (Zanzibar), Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda, Ethiopia, Djibouti, Eritrea, Somalia, Sudan na wenyeji Sudan Kusini.