HOFU ya kukosekana usiri na usalama kwa waathirika wa unyanyasaji na ukatili wa kijinsia katika vyuo vya elimu ya juu na maeneo mengine nchini, imepata suluhisho la kudumu, baada ya wanafunzi wawili kubuni mfumo wa kielektroniki, ambao pamoja na mambo mengine unazuia watu kupakazia wengine tuhuma za jinai.
Akizungumzia ubunifu huo jana, wakati wa maonyesho ya ubunifu wa stadi za kazi kwa wanafunzi (Carrier Fair), yaliyohusisha wanafunzi zaidi ya 100, amesema changamoto ya kuripoti matukio hayo kwa kutumia karatasi mtu anapokuwa Polisi, inawafanya waathirika wengi kuficha taarifa au kughairi kutoa taarifa wakihofia usalama wao.
Waliobuni mfumo huo, ni wanafunzi wa mwaka wa tatu wa Shahada ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Neema Costantine na Paschal Matiko.
Kwa mujibu wa Neema, mfumo huo unamsaidia mwathirika mwenyewe kuripoti taarifa yake kwa haraka kwenda Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi bila kufohia chochote, huku ukimhakikisha usiri na mtu haihitaji kuonekana au kwenda Polisi.
“Hili ni suala ambalo linasumbua sana ulimwengu mzima, lakini sisi tumejikita sana kwa upande wa wanafunzi wa vyuo vikuu, kwa sababu tumeona ndio eneo ambalo kuna mkusanyiko wa watu wengi ikiwemo vijana wa kike kwa wa kiume.
“Sasa hivi watu wanaipitia changamoto hii kwa asilimia kubwa sana, kwa hiyo tulitamani kufanya hiki kwa sababu hapo nyuma njia ambazo zinatumika kuripoti hizi kesi, ni mifumo ya traditionally; yaani mtu anaenda ofisini moja kwa moja, wakati mwingine kuna kuwa na mizunguko mingi mpaka kufikia kupata msaada.
…Lakini pia, wakati mwingine mtu anaweza akaogopa kwenda kuripoti yeye mwenyewe moja kwa moja. Kwa hiyo sisi tulitamani kutengeneza kitu ambacho kitamsaidia mtu kuripoti moja kwa moja.
Zaidi ameongeza: “Kwa hiyo hakuna haja ya yeye kuonekana lakini pia kwa wale wanmaohusika kutoa msaada ni muda wote, kwa maana ya saa 24 wana uwezo wa kupata notification ya taarifa ya mtu na wakatoa msaada wa haraka.
Na kingine watu wananyanyasika ila wanaogopa kutoa taarifa. Kwa hiyo mfumo huu utamsaidia mtu kuripoti taarifa yake kwa haraka bila kufohia chochote, inahakikisha kunakuwapo na usiri na mtu haihitaji kuonekana.”
Kutokana na ubunifu huo, Mhadhiri Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Dk. Cyril Komba, amesema baada ya serikali mwaka 2021 kuanzisha madawati ya kuripoti ukatili wa kijinsia kwenye vyuo vya elimu ya juu, wanafunzi hao walianza kazi ya kubuni mfumo utakaosaidia kupunguza matumizi ya karatasi.
Dk. Komba, amesema mfumo huo utasaidia kuondoa ukakasi au kumpakazia mtu tuhuma.
Mkurugenzi wa Huduma za Wanafunzi wa MoCU, Dk. Elisifa Nnko, amesema maonyesho hayo ni ya 12 kufanyika chuoni hapo.
Wakati, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho (MoCUSO), Yohana Kazimiri, aliishukuru menejimenti ya MoCU kwa kuruhusu wanafunzi wake kuonyesha vitu ambavyo wanavyo nje ya elimu ya darasani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED