Mwenda, Singida imeisha hiyo, atua kambini rasmi

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:50 AM Sep 09 2024
news
Picha: Mtandao
Beki Israel Mwenda.

BAADA ya mvutano wa muda mrefu, hatimaye beki Israel Mwenda amewasili kwenye kambi ya Klabu ya Singida Black Stars, imeelezwa.

Klabu hiyo, imemposti mchezaji huyo akiwa kambini huku mwenyewe akirekodiwa akisema amefika.

"Kwa sasa nipo kambini, nimefika, nipo na timu ya Singida Black Stars," alisema Mwenda kwa kifupi ambaye awali aligoma kujiunga nayo kwa madai ya kutaka amaliziwe kitita chake kilichosalia cha ada ya usajili, Sh. milioni 60.

Klabu hiyo kwenye mtandao wake wa instagram, umeposti video fupi ikimuonesha akiwa amevaa jezi ya klabu hiyo huku wakifanya naye mahojiano ambayo wanatarajiwa kuyarusha wakati wowote ule kwenye mitandao yao rasmi ya kijamii kuelezea kila kitu kilichotokea hadi pande zote mbili kumalizana na mchezaji huyo kuamua kurejea.

Dakika za mwisho za sakata hilo, klabu hiyo ilimtaka kuripoti kambini ndani ya saa 24 na wao kama klabu watamtimizia kile ambacho amekuwa akikidai.

Sakata hilo lilianza kwa Singida Black Stars kumtangaza mchezaji huyo kuwa ni mtoro na hajawasili kambini licha ya kumsajili.

Hata hivyo, mchezaji huyo aligoma akidai hawezi kwenda kambini mpaka watakapommalizia pesa yake hiyo ya usajili, baada ya awali kumpatia Sh. milioni 140, ambazo alizirejesha kwenye klabu yake ya zamani ya Simba.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Hussein Massanza, hakupinga hilo, ila alisema pesa hizo zilitakiwa kulipwa wakati akiwa tayari kambini, jambo ambalo lilipingwa na mchezaji mwenyewe ambaye alidai mmoja kati ya vipengele vya mkataba ni kummalizia pesa iliyobaki ili ajiunge na kambi.

Sakata hilo lilichukua nafasi kwenye vyombo vya habari kiasi cha wiki nzima, kabla ya jana kumalizika rasmi.

Mwenda ambaye tayari alikuwa ameshasajiliwa na Simba, aliomba kuondoka kwa kile kilichodaiwa kuwa hakutaka kucheza timu moja na beki mwenzake wa kulia, Shomari Kapombe, kwenye kikosi hicho, ambapo viongozi walimtaka aununue mkataba wake kwa Sh milioni 140 ili kuruhusiwa kuondoka.