Mutale apewa miaka mitatu Simba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 05:59 AM Jun 16 2024
Jushua Mutale.
Picha: Mtandao
Jushua Mutale.

SIKU moja baada ya dirisha la usajili kufunguliwa, hatimaye klabu ya Simba imefanikisha usajili wa winga machachari wa Power Dyamos ya Zambia, Jushua Mutale kwa kumsainisha mkataba wa miaka mitatu.

Habari za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo, zinasema kuwa mchezaji huyo, mwenye uwezo wa kucheza winga zote mbili, pamoja na namba 10, alikamilisha kutia saini jana jioni nchini Zambia, ambapo mkataba wake utamalizika Juni 2027.

Nipashe inafahamu siku tatu zilizopita mmoja wa watu waliopewa kazi ya kufanya usajili na Mwekezaji, Rais wa Klabu hiyo na Mwenyekiti wa Bodi, Mohamed Dewji alikwenda Zambia kukamilisha dili hilo.

"Nilikwambia kuwa jamaa aliyekuwa Zambia yuko katika hatua za mwisho, sasa ni rasmi, Mutale amesaini kuichezea Simba leo jioni (juzi), safari hii watu hawataki mchezo, hakuna mkataba wa miaka miwili, tukiwa na uhakika kuwa mchezaji huyo ni mzuri, umri mdogo na anaweza kutupa mafanikio, tunampa miaka mitatu," alisema kiongozi mmoja ndani ya klabu hiyo.

Inaelezwa kuwa mchezaji huyo anakuja kuchukua nafasi ya Luis Miquissone ambaye ameshindwa kuonyesha makali yake tangu aliporejea kutoka Al Ahly ya Misri mwanzoni mwa msimu huu, huku tetesi zikisema tayari UD Songo ya nchini kwao, Msumbiji imeonyesha nia ya kutaka kumrudisha nyumbani nyota huyo.

Mutale, raia wa Zambia, aliwachachafya mabeki wa Simba, hasa Shomari Kapombe, katika mechi ya tamasha la Simba Day iliyochezwa Agosti 6 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba ikishinda mabao 2-0, lakini pia aliwafanya anavyotaka katika mchezo wa raundi ya kwanza, Ligi ya Mabingwa Afrika, Septemba 16 mwaka jana nchini Zambia, timu hizo zikitoka sare ya mabao 2-2, na alikuwa mwiba kwa mara nyingine katika mechi ya marudiano, Oktoba Mosi, mwaka jana,  Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam timu hizo zikitoka sare ya bao 1-1 na Simba kutinga hatua ya makndi kwa faida ya mabao mengi ya ugenini.

Baadhi ya wachezaji wanaotajwa kuwa huwenda wakatua Msimbazi ni  winga mwingine anayeichezea klabu ya AS Vita ya  Jamhuri ya Kidemkorasi ya Congo, Elie Mpanzu, mshambuliaji Derrick Fordjour kutoka Medeama ya Ghana.

Pia imetajwa kumuwinda mshambuliaji Ricky Banda, raia wa Zambia anayeichezea Red Arrows ya nchini humo,  mlinzi wa kati wa Mamelodi raia wa Kenya, Brian Mandela Onyango, mshambuliaji Agostinho Mabululu raia wa Angola anayechezea klabu ya Al Ittihad ya Misri, na kiungo mkabaji Ibrahim Gadiaga wa FC Nouadhibou ya Mauritania.

Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo Ahmed Ally, ametangaza rasmi kuwa kuanzia kesho Jumatatu wataanza kutangaza wachezaji walioachwa, wakifuatiwa na wale walioongeza mikataba, kabla ya kutangaza wapya waliosajiliwa.

Amesema wachezaji, watakaoachwa ni wale ambao viwango vyao haviridhishi, umri mkubwa, majeraha sugu na utovu wa nidhamu.

"Kikubwa ambacho watu wanataka kusikia ni nani anaondoka ndani ya klabu na nani anaingia, taarifa zote muda si mrefu zitaanza kutoka, kuanzia Jumatatu tutaanza kutoa taarifa ya wale wanaoondoka, baadaye tukimaliza, tutakuja na wale ambao wameongeza au tumewaongezea mikataba, mwisho kabisa tutaanza sasa taarifa rasmi za usajili," alisema Meneja Habari huyo.

Alisema imewalazimu safari hii kufanya upembuzi yakinifu, tathimini na umakini wa hali ya juu kumuangalia mchezaji mmoja mmoja na mchango wake katika timu.

"Kila mmoja anafahamu tumefanya vibaya msimu uliopita kwa hiyo ni lazima kwanza ufanyike upembuzi yakinifu, kwa sasa tumeshamaliza kupitia ripoti ya walimu wote, waliopita na waliopo, kitu gani wamependekeza na nini kifanyike kwa ajili ya msimu ujao, kilichobaki ni utekelezaji wa hizo ripoti," alisema Ahmed.