KIKOSI cha Mashujaa FC kimeweka kambi Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa raundi ya tatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Pamba Jiji utakaochezwa Septemba 21, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Kocha Mkuu wa Mashujaa, Mohamed Abdallah 'Bares' amesema baada ya mapumziko ya wiki moja, timu yake imeanza mazoezi ili kujiimarisha kuelekea mchezo huo utakaokuwa na upinzani.
Bares alisema licha ya kutopoteza mechi, anarejea kwenye uwanja wa mazoezi kuimarisha sehemu ambazo amebaini zinahitaji kuboreshwa.
"Tulipata mapumziko ya wiki moja, sasa tunarejea kambini kujiandaa na mchezo mwingine wa Ligi Kuu, tumecheza mechi mbili mpaka sasa, kuna mazuri yapo, lakini pia kuna mapungufu nimeyaona, nakwenda kuyarekebisha," alisema kocha huyo.
Mashujaa ilianza msimu mpya Agosti 17, mwaka huu kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji, shukrani kwa straika wa zamani wa Yanga, Crispin Ngushi kufunga huku Agosti 23, mwaka huu ililazimishwa suluhu na Maafande wa Prisons.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED