MZEE Juma Magoma ametoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam mikono nyuma huku akiwa ameshika chupa ya maji ya lita moja, baada ya rufaa aliyokata dhidi ya uamuzi mdogo uliyoipa ushindi Bodi ya Wadhamini wa Klabu ya Yanga kutupiliwa mbali.
Aidha, Magoma akiwa mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Livini Lyakinana, muda wote alikuwa ameweka mikono yake kwenye mdomo wake na macho yake yakiwa yanamwangalia msajili huyo wakati anasoma hukumu hiyo hadi mwisho.
Akisoma uamuzi huo, Lyakinana kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Salma Maghimbi, aliyesikiliza rufaa hiyo, alisema uamuzi mdogo waliokuwa wanaupinga Magoma na wenzake haukatiwi rufaa.
"Uamuzi waliokuwa wanaupinga haukatiwi rufaa kwa mujibu wa sheria, rufaa inatupiliwa mbali," alisema Lyakinana wakati akisoma uamuzi huo kwa niaba ya jaji huyo.
Wakati wakiwasilisha hoja zao Wakili wa Yanga, Kalagho Rashid, aliwasilisha hoja za pingamizi la awali akipinga rufani iliyokatwa na wazee hao kwamba haipaswi kukatiwa rufaa kwa mujibu wa sheria.
"Haki za msingi za wadaawa ziliamuliwa katika shauri la marejeo ambalo pande zote mbili zilisikilizwa na wadaawa waliwakilishwa na mawakili wao, hivyo uamuzi huo haupaswi kukatiwa rufani," alidai Wakili Rashid
Alidai kuwa rufaa hiyo imeshapitwa na tukio kwa kuwa tayari Mahakama ya Kisutu imeshasikiliza maombi yao ya marejeo na kutengua hukumu yake ya awali hivyo hakuna chochote kinachoweza kubadilishwa hata kama rufaa yao ikikubaliwa.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa Magoma, Jacob Mashenene, alidai uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kisutu unaamua haki za msingi za wadaawa kwa sababu hakuna shauri lolote lililobaki mahakamani baada ya uamuzi uliotolewa.
Wakili Mashenene alidai kuwa hoja ya rufaa hiyo imepitwa na wakati, alidai kuwa hoja hiyo haifai kuwa hoja ya pingamizi kwa sababu mahakama itatakiwa kutafuta ushahidi kuthibitisha hilo.
"Naomba mahakama itupilie mbali pingamizi la awali lililowasilishwa na Bodi ya Wadhamini Yanga na rufaa yao iendelee kusikilizwa,"alidai Mashenene
Magoma na mwenzake wanapinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu uliokubali ombi lao la bodi hiyo kufungua nje ya muda maombi ya marejeo ya hukumu iliyobatilisha Katiba ya Klabu hiyo ya mwaka 2010.
Aidha, Magoma na mwenzake wamekata rufaa hiyo dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Klabu ya Yanga, ambayo ndio mjibu rufaa wa kwanza.
Wajibu rufaa wengine ni waliowahi kuwa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Klabu hiyo, Fatma Abeid Karume ( bado mjumbe mpaka sasa), Abeid Abeid na Jabiri Katundu (mjibu rufaa wa pili, wa tatu na wa nne mtawalia).
Wamekata rufaa hiyo wakipinga uamuzi huo wa Mahakama ya Kisutu kwa madai kuwa iliwapa wadhamini hao wa Yanga ruhusa ya kufungua maombi hayo ya marejeo ya hukumu hiyo bila wao kupewa nafasi ya kusikilizwa katika maombi hayo ya Yanga.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED