KOCHA wa timu ya Inter Zanzibar FC, Abrahaman Mohamed amesema kupoteza mchezo wao wa kwanza wa Ligi kuu ya Zanzibar juzi kumetokana na ugeni wao kwenye Ligi hiyo.
Inter Zanzibar FC ilijikuta ikipokea kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa bingwa mtetezi, JKU SC, katika mchezo uliochezwa juzi katika uwanja wa New Amaan Complex Visiwani hapa.
Akizungumza na gazeti hili, Mohamed alisema walicheza na timu yenye uzoefu mkubwa katika soka la Zanzibar lakini pia iliyopata kucheza mashindano mawili ya kimataifa hivi karibuni 'klabu Bingwa na Kagame cup'.
Alisema kupitia mashindano hayo walifanikiwa kupata maandalizi mazuri ya kujiandaa na msimu hivyo matokeo aliyoyapata hayawezi kumshangaza.
Alisema wachezaji wake walicheza vizuri katika kipindi cha kwanza lakini kipindi cha pili walishindwa kwenda sawa na wapinzani wao na kujikuta wakipata kipigo hicho.
"Wapinzani wetu walicheza kwa mipango kwa kutumia uzoefu wao ndani ya ligi jambo ambalo wachezaji wangu walishindwa kwenda nao sawa, tumefungwa kwa sababu ya ugeni wetu kwenye Ligi," alisema Mohamed.
Aidha alisema mbali na ugeni wa Ligi lakini pia wachezaji wake wengi walikuwa na hofu ya mchezo jambo lilowafanya kushindwa kucheza vizuri.
"Mchezo huu hatukufanya vizuri lakini kupitia mchezo huu nimeona mapungufu yapo wapi hivyo katika mchezo wetu wa pili dhidi ya Malindi SC tutakuwa bora zaidi," alisema.
Hata hivyo alisema kuwa kazi iliyombele yake katika kukiboresha kikosi chake ni kuhakikisha anawatoa uoga na hofu ya mchezo bila kujali historia ya timu wanayocheza nayo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED