BAADA ya kuanza vibaya Ligi Kuu kwa kupoteza michezo yote miwili ya mwanzo, kikosi cha Kagera Sugar leo kina kibarua kingine cha kusaka alama tatu dhidi ya Tabora United.
Kagera itakuwa ugenini kwenye mchezo huo na kocha wa timu hiyo, Paul Nkata, amesema wanataka kuanza kukusanya pointi kuanzia kwenye mchezo huo.
"Hatuna rekodi nzuri kwenye michezo yetu miwili iliyopita, lakini tumeendelea kujiimarisha na kufanyia kazi mapungufu yetu, naamini kuanzia mchezo wa kesho (leo), tutaanza kupata matokeo mazuri," alisema Nkata.
Alisema moja ya sababu iliyowafanya kushindwa kuvuna pointi kwenye michezo yao miwili iliyopita, ni umakini mdogo kwenye kuzitumia nafasi wanazozitengeneza.
"Tumekuwa tukicheza vizuri na kujitahidi kutengeneza nafasi za kutosha, lakini tumekuwa na umaliziaji mbovu, hili nililiona na tumekuwa tukilifanyia kazi kwenye uwanja wa mazoezi," alisema Nkata.
Aidha, alisema katika mazoezi ya hivi karibuni, safu yake ya ushambuliaji imeendelea kuimarika na kuonesha matumaini ya kupata mabao kwenye michezo inayofuata.
Kikosi hicho cha Kagera juzi kilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Geita Gold na kuambulia sare ya bao 1-1.
Katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu inayorejea tena leo, Fountain Gate itaumana na Kengold FC na kufanya leo kuwa na michezo miwili ya ligi hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED