BAADA ya timu ya JKU kutwaa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Chipukizi FC mabao 2-0 kwenye mechi iliyochezwa Uwanja wa New Amaan Complex juzi, 'Wajeda' hao wamesema sasa wamebakiza malengo makubwa mawili ndani ya msimu huu 2024-2025 ili kuwa wa furaha zaidi kwao.
JKU ilifanikiwa kutetea taji hilo la Ngao ya Jamii, wakilitwaa kwa mara ya pili mfululizo katika mchezo huo mkali uliopigwa juzi uwanjani hapo.
Akizungumza na gazeti hili baada ya mechi hiyo, Kocha wa timu hiyo, Salum Haji, alisema bado mipango yao miwili imebakia ili kuhakikisha msimu huu hawafanyi makosa kama uliopita.
Alisema walichobakisha ni kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu pamoja na kuhakikisha wananyakuwa Kombe la Shirikisho la Soka la Zanzibar, maarufu FA Cup.
Haji alisema mipango yao mikubwa ni kunyakuwa mataji yote matatu na kwamba tayari wameanza na Ngao ya Jamii, hivyo kinachofuata ni kujipanga kwa hayo mawili yaliyosalia.
"Tunaunza msimu kibabe zaidi kama ilivyokuwa kwa msimu uliopita. Msimu huu ni kuhakikisha hakuna tutakachokiacha katika mashindano ambayo tunashiriki," alisema.
Aidha, akizungumzia mchezo huo wa Ngao ya Jamii, alisema haukuwa rahisi, lakini lengo la kutetea taji hilo wamefanikiwa.
Alisema kulingana na uwezo wa kiuchezaji kwa wachezaji wake hana hofu katika michezo ya Ligi Kuu Zanzibar ambayo itaanza rasmi Ijumaa wiki hii.
Alisema kikosi chake kimepata maandalizi ya kutosha kulingana na mashindano waliyoshiriki hasa michuano ya Kombe la Kagame iliyofanyika Tanzania Bara hivi karibuni.
"Mchezo ulikuwa mgumu, lakini wachezaji wangu wamepata uzoefu zaidi, wamecheza kwa mipango na malengo mpaka tumepata ushindi," alisema Haji.
Hata hivyo, alisema licha ya kuwa na wachezaji majeruhi watatu wa kikosi cha kwanza na wanaotegemewa, lakini timu yake ilicheza vizuri na haikuwa na hofu ya mchezo.
Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu Zanzibar iliyotangazwa mwishoni mwa wiki na Bodi ya Ligi visiwani humo, Mabingwa Watetezi, JKU Ijumaa wiki hii watakata utepe wa kinyang'anyiro hicho dhidi ya Wanagenzi Inter Zanzibar ambao wamepanda daraja msimu huu, mchezo ukitarajiwa kupigwa Uwanja wa New Amaan Complex
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED