JKT Queens kambini mapema kwa Ligi Kuu

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 07:00 AM Sep 04 2024
Ofisa Habari wa timu hiyo, Masau Bwire.
Picha:Mtandao
Ofisa Habari wa timu hiyo, Masau Bwire.

KATIKA kuhakikisha msimu huu hakifanyi tena makosa kwenye mbio za ubingwa, Kikosi cha timu ya JKT Queens, kimeanza kambi mapema kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu ya Wanawake.

Msimu uliopita JKT Queens, ilipoteza taji la ligi hiyo dhidi ya Simba Queens, ambayo pia ilizoa alama zote sita dhidi ya miamba hiyo ya jeshi.

Akizungumza na Nipashe jana, Ofisa Habari wa timu hiyo, Masau Bwire, alisema wameamua kuanza kambi mapema ili msimu ujao wabebe ubingwa wa ligi hiyo. 

"Huwa ni kawaida yetu kuanza maandalizi mapema kwa kuwa tuna malengo ya kufanya vizuri zaidi msimu ujao ili tubaki na ubingwa," alisema Bwire.

Aliongeza kuwa kikosi kipo imara kuhakikisha kinapata matokeo mazuri kwenye michezo yao yote watakayoicheza msimu ujao.

Aidha, alisema kutokana na aina ya wachezaji waliopo katika kikosi hicho ana matumaini makubwa ya kupata matokeo mazuri kwenye mechi zao ligi itakapoanza. 

Alisema kabla ya msimu kuanza watacheza michezo ya kirafiki huku wakiwa wana subiri ratiba itolewe ili wajue wanaanza na nani.

Aliwataka mashabiki wao kuendeleakuwapa ushirikiano kama walivyofanyia msimu uliopita ili watimize malengo yao.