Hatima Yanga robo fainali Afrika kesho

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:46 AM Jan 11 2025
Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic.
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amesema amewaandaa wachezaji wake kimwili, kiakili na kiufundi kwa ajili ya mchezo wa raundi ya tano, Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan, utakaopigwa kesho saa 4:00 kwenye Uwanja wa De la Capitale, jijini Nouakchott, nchini Mauritania.

Akizungumza akiwa nchini humo, Ramovic, alisema mchezo wa kesho ndiyo unashikilia hatima yao na wamejiandaa kuhakikisha wanashinda ili kujiweka katika mazingira mazuri kwenye mchezo wa mwisho utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam dhidi ya MC Alger ya Algeria, Januari 18, mwaka huu.

"Kwa sasa hatuwezi kuangalia matokeo ya mechi zingine, tunachotakiwa ni sisi wenyewe kuangalia kwanza tunafanya nini. Tunahitaji ushindi kwa hali na mali kwenye mchezo huu. Tukishinda tutakuwa na pointi saba ambazo zitatusogeza na kuangalia nini tutafanya katika mchezo wa mwisho," alisema kocha huyo.

Matokeo yoyote tofauti ya ushindi, yanaweza kuiweka kwenye hali ngumu zaidi Yanga ya kusonga mbele kwenye hatua ya robo fainali.

"Nimewaandaa vijana wangu kimwili, kiakili na kiufundi kwa ajili ya mchezo huu na wachezaji wanajua kuwa wanapaswa kushinda tu kama wanataka tusonge mbele," alisema kocha huyo.

Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe alisema tangu watue nchini humo hawajapata usumbufu wowote au dalili ya kuonyesha kuwa kuna hujuma dhidi yao, huku akisema hali ya hewa ni baridi ya kawaida ambayo haiwezi kuwazuia kucheza kwa ubora wao.

"Hakuna baridi ya kutisha kama ya Tunisia au Algeria, hatujagandishwa sana Uwanja wa Ndege, au kufanyiwa hujuma yoyote, kusema kweli kila kitu kimekwenda safi, tunachosubiri ni dakika 90 tu za mchezo," alisema Kamwe.

Ikumbukwe kuwa, Al Hilal inacheza mechi zake nchini Mauritania kutokana na Sudan kukabiliwa na machafuko.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Al Hilal, Florent Ibenge, amesema mchezo wao dhidi ya Yanga siyo muhimu sana kwao, lakini anategemea kupata upinzani mkali kutoka kwa wapinzani wao kwa kuwa ni mchezo wanaouhitaji kupata matokeo mazuri.

"Niwapongeze wachezaji wangu kwa kazi ngumu na kubwa waliyoifanya katika michezo ya mwanzo, naamini tulitumia nguvu kubwa tofauti na michezo tunayoenda kucheza sasa presha itakuwa kwa wapinzani wetu.

Niseme tu kuwa, Yanga ya msimu uliopita siyo kama ya msimu huu, ubora wao umepungua, sisi tumefuzu, hatima yao ipo mikononi mwetu wafuzu au tuwatoe klabu bingwa.

Malengo yetu ni kumaliza tukiongoza kundi haitokuwa mechi rahisi kwao, wajipange," alisema Ibenge, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.