Gamondi: Ni ngumu kushinda tena tano

By Adam Fungamwango ,, Saada Akida , Nipashe
Published at 09:17 AM Apr 23 2024
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi.

BAADA ya kuwasambaratisha watani zao wa jadi Jumamosi iliyopita kwa mabao 2-1, Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, leo saa 10:00 jioni watashuka kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam kuwavaa Maafande wa JKT Tanzania.

Yanga itakuwa na kazi mbili, moja ni kusaka pointi tatu ili kuukaribia Ubingwa wa Tanzania Bara, lakini pia kutaka kuendeleza ubabe ambao iliufanya mechi ya mzunguko wa kwanza, ikiishindilia mabao 5-0, mechi iliyochezwa Agosti 29, mwaka jana, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, na kuzima ngebe za msemaji wa klabu hiyo, Masau Bwire, ambaye ameahidi kuwa watalipiza kisasi.

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema haamini kama wanaweza tena kufunga idadi kubwa ya mabao kama ilivyokuwa mzunguko wa kwanza, kwa sababu anafahamu wapinzani wao watakuja kivingine.

"Hakuna mechi rahisi, tunacheza kwa ajili ya kushinda na kutafuta pointi tatu, si kushinda mabao mengi, ikitokea nafasi ya kufunga zaidi tutafanya hivyo, mechi ya kwanza tulishinda mabao 5-0, nakumbuka kuwa tulicheza Azam Complex siyo huku tunakocheza, leo, tunatumia uwanja mwingine, hatufahamu kama utakuwa rafiki, kikubwa sisi tunahitaji pointi tatu tu,” alisema Gamondi.

Kocha huyo alisema kikosi chake hakikuwa na maandalizi ya kutosha kwa mechi ya leo, tangu walipocheza dhidi ya Simba Jumamosi iliyopita, ila tu wachezaji wake wamefanya mazoezi ya kujiweka sawa.

Aliwataja wachezaji ambao watakosekana katika mechi ya leo ni Joyce Lomalisa ambaye aliumia katika mchezo wa dabi, na Pacome Zouzoua ambaye bado mpaka sasa hajaanza kucheza mechi yoyote tangu alipoumia, Machi 17, mwaka huu, katika mechi ya Ligi Kuu kati ya timu hiyo na Azam FC.

Kocha Msaidizi wa JKT Tanzania, George Mketo, alisema kikosi chake kipo tayari kwenda kukutana na timu kubwa ambayo imetoka kufanya vema mechi iliyopita, hivyo watacheza kwa tahadhari kubwa.

"Kila mchezo unakuja na mipango yake mechi ya kwanza tulifungwa 5-0,  mechi hii ni nyingine na tumejipanga vizuri kutumia vizuri uwanja wetu wa nyumbani na hatupo vizuri katika msimamo wa ligi, hivyo inabidi tupambane," alisema Mketo.

JKT Tanzania haijashinda mechi yoyote ile ikicheza uwanja wake huo wa nyumbani, ikicheza nne na kupoteza moja, ikiaanza kwa kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Simba, kabla ya kulazimishwa suluhu dhidi ya Namungo, ikatoka sare ya bao 1-1 dhidi ya KMC, na nyingine kama hiyo dhidi ya Prisons, huku ikishika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi, ikiwa na pointi 22.