LICHA ya kuchora ramani nzuri ya kutwaa taji la ubingwa kwa msimu huu, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, ameendelea kusisitiza kuwa wanahitaji kupambana na kujitoa katika michezo iliyosalia ya mzunguko huu wa lala salama Ligi Kuu Tanzania Bara ili kufikia malengo hayo.
Amesema anaimani wametoka kwenye michezo migumu, lakini anaamini wanapoelekea ni zaidi ya walipotoka hasa katika michezo saba iliyosalia ya Ligi hiyo kuhakikisha wanavuna pointi muhimu katika kila mchezo uliopo mbele yao.
Gamondi alisema hayo juzi baada ya kukamilika kwa dakika 90 za mchezo wa Kariakoo 'Derby' kwa kufanikiwa kuvuna pointi tatu zingine mbele ya watani wao wa jadi, Simba kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2 -1, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Alipongeza utendaji kazi mzuri wa kundi lake la wachezaji kwa tabia ya kupambania timu.
“Mambo muhimu zaidi ni kucheza ndani ya uwanja, bila shaka tumefanikiwa mipango yetu, najivunia wachezaji wangu maana hata kwa nyakati ambazo hawachezi vizuri, lakini wanapambana kupata matokeo mazuri,” alisema Kocha huyo.
Aliongeza kuwa haikuwa mechi rahisi, lakini anajivunia kiwango cha wachezaji wake katika kila mechi ikiwamo hiyo ya Derby kwa kucheza kwa tahadhari na kuwaheshimu wapinzani wao, hivyo kufanikiwa kuvuna pointi tatu zingine.
Kuhusu ubingwa, alisema licha ya kupata mwanga nzuri, lakini hawajihakikishii kwa sababu bado wana michezo takriban saba iliyopo mbele yao na anaamini ni migumu kuliko ambayo wametoka kucheza.
“Hatuna uhakika kwa asilimia zote kwa sababu tuna mechi za ushindani, tunacheza Jumamosi nyumbani halafu tunaenda kucheza ugenini, tunahitaji kupata pointi muhimu katika hizo mechi ili kufikia malengo yetu,” alisema Gamondi
Mshambuliaji wa Yanga, Joseph Guede alisema anafurahi kufunga bao la ushindi katika mchezo huo wa Derby, jambo ambalo linampa mwanga wa kuendelea kufanya hivyo kila anapopata nafasi.
Naye Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, alisema mechi ilikuwa nzuri na ngumu kipindi cha kwanza dakika 10, waliweza kutengeneza nafasi mbili, shida lakini bado iko palepale.
“Bado tatizo letu halijapata majibu tumetengeneza nafasi, lakini kuzigeuza kuwa mabao ni ngumu, pia tulilazimika kufanya mabadiliko ya lazima baada ya Henock Inonga kuumia na mchezaji aliyekuja kuchukuwa nafasi yake akasababisha penalti na kuwapinzani kupata bao la kwanza.
"Kuhusu ubingwa ni ngumu sana, lakini bado tunatakiwa kupambana kushinda katika mechi zilizosalia. Baada ya kuwa nyuma ya bao mbili tulilazimika kuongeza watu mbele ili kuweza kupata bao na kufanikiwa kufunga moja,” alisema Matola.
Na kuhusu safu ya ulinzi alisema bado wamekuwa wakiruhusu bao katika kila mechi jambo ambalo wataendelea kulifanyia kazi katika sehemu zote za mapungufu wakiiandaa na michezo iliyosalia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED