KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema yeye na wachezaji wake msimu huu ni lazima wapambane zaidi kwenye michuano mbalimbali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Tanzania Bara, kwani timu zote zimejiandaa kutaka kuwafunga.
Gamondi ambaye kikosi chake kinajiandaa kwenda kucheza mechi ya raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CBE ya Ethiopia, alisema amewaambia wachezaji wake kuwa wasijidangaye kuwa wapo kwenye mstari salama, badala yake kiwango kikubwa walichoonesha msimu uliopita kimewafanya kukamiwa zaidi na kila timu itakayokutana nayo kwenye Ligi ya Mabingwa na Ligi Kuu Tanzania.
"Kila timu sasa inataka kuifunga Yanga, inabidi tupambane, tusijidangaye kuwa tupo kwenye mstari salama, ninawaambia haya hata wachezaji wangu, wanatakiwa kila siku waongeze juhudi na mazoezi zaidi ili tuwe bora kila kukicha kwani wenzetu nao wanaongeza ubora ili watufikie au watupite," alisema Gamondi.
Alisema kwenye soka siku zote mwalimu ni lazima ujiongeze na kwani kuna presha ambayo inakusukuma ili ufanye vema.
"Na si kwenye soka tu, hata kwenye maisha ni lazima uwe na presha ya kusaka maisha, kuweza kulipa kodi, kutunza nyumba, kulisha watoto, kuwalipia ada, yote hii ni presha na hiyo ndiyo inakufanya uwe makini na ujitume.
"Kwa mfano sisi makocha kazi yetu ni ngumu, kosa moja la mwamuzi linaweza kubadilisha matokeo yote ya mchezo, timu ikafungwa, kocha ukajikuta huna kazi kwa kosa la mtu mwingine," alifafanua kocha huyo.
Hata hivyo, Gamondi ameelezea kufuarahishwa na kufahamu tabia za wachezaji wake wengi baada ya msimu mmoja kupita.
Alisema msimu uliopita alipata tabu sana kujua mazingira na aina ya wachezaji anaofanya nao kazi, lakini kwa sasa hana wasiwasi.
Nina furaha sana msimu huu, uliopita nilipata tabu, nilikuwa sijui vitu vingi, siwajui wachezaji ninaofanya nao kazi, siwajui aina ya wachezaji wanaocheza Ligi Kuu ya Tanzania, lakini sasa naelewa vitu vingi.
Kingine msimu huu nina wachezaji wapya sita wenye viwango vya juu ambao unaweza kufanya mabadiliko usiwe na presha yoyote, ingawa pamoja na hayo siwezi nikaahidi makubwa sana kwa sababu bado msimu ni mpya kwa mashindano yote," alisema kocha huyo raia wa Argentina.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED