Gamondi aiweka CBE kiganjani kwake

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:07 AM Sep 08 2024
KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi
Picha: Mtandao
KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amemaliza kuwapeleleza wapinzani wake CBE, na sasa anasubiri siku ifike ili aoneshe kile alichokisoma kwao.

Yanga itacheza mechi ya raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya timu inayomilikiwa na Benki ya Ethiopia, CBE, katika mchezo wa mkondo wa kwanza utakaochezwa, Uwanja wa Abebe Bikila, jijini Addis Ababa, Jumamosi ijayo.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kocha huyo ambaye alikuwepo Jumatano iliyopita, Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mchezo kati ya Taifa Stars dhidi ya Ethiopia, pamoja na mambo mengine alikwenda kuwaangalia baadhi ya wachezaji wa CBE ambao wanaichezea timu yao ya taifa.

"Alifanya vitu viwili kwa wakati mmoja, alikwenda kuiangalia Stars, lakini alikuwa na majina na namba za mgongoni za wachezaji wa CBE wanaoichezea timu ya taifa, lengo ni kuangalia viwango vyao na jinsi wanavyocheza ili iwe rahisi kuwaelekeza wachezaji wa Yanga jinsi ya kukabiliana nao," alisema mtoa taarifa.

Baada ya mchezo huo, Gamondi hakutaka kuongea chochote na waandishi wa habari.

mbali na hilo, habari zinasema alimtuma mmoja kati ya wachambuzi wa video kwenda kuangalia michezo miwili kati ya CBE na SC Villa ambayo ilichezwa nchini Uganda, Uwanja wa Mandela, Agosti 17 na Abebe Bikila uliopigwa Agosti 24.

Katika mchezo wa kwanza ikiwa ugenini, CBE ilishinda mabao 2-1, na mechi ya marudiano nyumbani ilitoka sare ya bao 1-1.

"Alitumwa mtaalam kuangalia mechi hizo kwa sababu yoyote ambaye angeshinda angekutana na Yanga, na baada ya CBE kupita kazi ilianza ya kuichambua jinsi inavyocheza, kizuri zaidi na baadhi ya wachezaji wao wamekuja hapa na kikosi cha Ethiopia, mwenyewe alikwenda kuwaangalia.

Kwa maana hiyo tayari ameshaifahamu timu hiyo jinsi inavyocheza na nini anatakiwa afanye yeye na wachezaji wake," kilisema chanzo hicho.

Hivi majuzi, Gamondi alisema watakwenda kucheza ugenini kwa tahadhari na kuwadhibiti wapinzani wao ili wasipate ushindi kabla ya kuwamalizia nchini Tanzania.

"Tukimaliza kuwapeleleza, tutakwenda kucheza mechi ya kwanza ugenini, tutajaribu kuwadhibiti kwanza kwao, tukifanikiwa kuwasukuma na kuwadhibiti ili wasitufunge, tutakuja kuwamalizia huku kwenye mchezo wetu wa nyumbani  na kufuzu makundi," alisema Gamondi.

Mechi ya marudiano inatarajiwa kuchezwa Dar es Salaam kati ya Septemba 20 mpaka 22, ambapo mshindi kati ya timu hizo mbili atatinga hatua ya makundi.