Gamondi afuta mapumziko Yanga, Baleke kimeeleweka

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:28 AM Sep 03 2024
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe
Picha:Mtandao
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, ameamua kutovunja kambi, badala yake ameendelea na mazoezi na kikosi kilichobaki, baada ya wachezaji 14 wa timu hiyo kuondoka kwenda kujiunga na vikosi mbalimbali vya timu za taifa kwa ajili ya michezo ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe, alisema jana kuwa, awali walidhani anaweza kuvunja kambi na kuwaita baadaye kutokana na kuondokewa na wachezaji wengi, lakini  Gamondi amekataa, badala yake ameendelea na wachezaji aliobaki nao kwa ajili ya kujindaa na mchezo wa raundi ya kwanza, Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CBE ya Ethiopia.

Baada ya Kalenda ya FIFA, klabu nyingi zimewapa mapumziko ya muda mfupi wachezaji wao kabla ya kurejea tena kuendelea na kambi.

"Tupo kwenye mapumziko ya timu za taifa, sisi tumetoa wachezaji 14 kwenda kwenye vikosi vya timu za taifa na tunawatakia kila laheri na waliobaki wanaendelea na mazoezi, baada ya Kalenda ya FIFA kumalizika kutakuwa na siku tatu au nne kabla ya mechi, hivyo kocha hajavunja kambi, wachezaji wanaendelea na mazoezi na wachezaji waliobakia.

Tunaamini tuna kikosi bora hata hawa waliobaki wataandaliwa vema ili waje kuungana na wengine watakapotoka kwenye timu zao za taifa kwa ajili ya mchezo wetu muhimu," alisema Kamwe.

Yanga inatarajia kucheza mchezo wa mkondo wa kwanza kwenye Uwanja wa Abebe Bikila nchini Ethiopia dhidi ya wapinzani wao, timu inayomilikiwa na Benki Kuu nchini humo, kabla ya mechi ya marudiano inayotarajiwa kuchezwa, Septemba 20, mwaka huu, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kamwe pia alitoa ufafanuzi kwa nini straika mpya wa timu hiyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Jean Baleke, amekuwa haonekani kwenye kikosi hicho, akisema awali tatizo lilikuwa ni vibali, baadaye ikaja changamoto ya Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC), lakini kwa sasa limashamalizwa.

"Ni kweli hajaonekana, kwanza kulikuwa na tatizo la vibali,  baadaye alikosa mechi mbili za hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika, ITC zilichelewa, lakini kwa sasa kila kitu kiko sawa, alikosa mechi ya Kagera kwa sababu ya mahitaji ya kiufundi tu, mwalimu aliona aliosafiri nao wanamtosha kwa mechi ile na si yeye tu aliyebakia Dar es Salaam, ni wengi tu," alisema Kamwe.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa bado ni mapema sana kwani Yanga ina mashindano mengi na inahitaji wachezaji wengi wenye viwango vya juu, hivyo ana uhakika kuwa atatumika kutokana na mahitaji ya mwalimu.

"Itoshe kusema tuna michezo mingi sana msimu huu na ndiyo kwanza ligi inaanza, inahitajika kuwa na wachezaji wengi wenye uwezo, kwa hiyo anaweza kutumika sana huko mbele ya safari," alisema.

Beleke, awali alikuwa Simba na ilimuacha katikati ya dirisha dogo la msimu uliopita ambapo alitimkia Klabu ya Al Ittihad Tripoli ya Libya kabla ya kuibukia Yanga.