KOCHA Mkuu wa Fountain Gate, Mohamed Muya, amewaita mashabiki wa soka mkoani Manyara ili kuwashangilia katika mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KenGold utakaochezwa Septemba 11, mwaka huu kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa kwa sababu watawapta zawadi ya ushindi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Muya, alisema mechi hiyo itakuwa ni siku maalumu kwa mashabiki wao kwa sababu watacheza uwanjani hapo kwa mara ya kwanza na wanataka kuanza na historia nzuri ndani na mkoa huo.
Muya alisema pia wanataka kuweka rekodi ya kushinda mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu mkoani humo.
"Hivi sasa tupo mazoezini, tunajipanga kwa ajili ya mechi ya KenGold, vijana wote wapo imara, itakuwa ni mechi ya kwanza kucheza tukiwa hapa Manyara kwa sababu mechi zetu mbili tulicheza tukiwa nje, itakuwa ni siku maalum kwa mashabiki wa hapa na vitongoji vyake, tunawaomba wajitokeze kwa wingi wa sababu tunataka kuwapa zawadi ya ushindi, ili historia iandikwe kama ya kwanza ligi imechezwa na tumeshinda," alisema Muya.
Fountain Gate iliyoko katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi tatu ilianza msimu kwa kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Simba lakini ikapata ushindi magoli 2-0 ugenini dhidi ya Namungo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED