Fadlu aleta mfumo mpya Simba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:48 AM Sep 06 2024
KOCHA wa Simba, Fadlu Davids
Picha:Mtandao
KOCHA wa Simba, Fadlu Davids

KOCHA wa Simba, Fadlu Davids kwa siku za karibuni amekuwa akiwapa wachezaji wake mbinu katika mfumo mpya ambao anataka wawe wanapiga mashuti ya nguvu langoni pale wanapoona ngome ya mpinzani ni ngumu kupitika.

Katika mazoezi ya timu hiyo yanayofanyika kwenye uwanja wa Mo Arena, Bunju, Fadlu ameonekana akiwahimiza wachezaji wake kupiga mashuti kila wanapopata nafasi ya kufanya hivyo na kupunguza aina yao ya uchezaji ya kutaka kuingia mpaka kwenye boksi.

Simba inajiandaa na mechi ya raundi ya kwanza, Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Tripoli mchezo utakaochezwa ugenini Septemba 15 kwenye Uwanja wa Juni 11, kabla  ya marudiano, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Septemba 20 mwaka huu.

Kocha huyo raia wa Afrika Kusini alikuwa akiwatumia wachezaji, Awesu Awesu, Debora Fernandes, Jean Ahoua, Leonel Ateba na Valentino Mashaka kwa ajili ya kupiga mashuti ya mbali.

Mbali na aina hiyo ya mazoezi, kocha huyo pia aliwaelekeza wachezaji wake jinsi gani ya kumalizia mipira ya krosi, ambapo aliwatenga baadhi ya wachezaji kwa ajili ya kupiga mashuti na wengine kumalizia kwa miguu na vichwa.

Katika mazoezi hayo, kiungo Fabrice Ngoma, ambaye amerejea ndani ya kikosi hicho baada ya kutoka kwao, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, alipokwenda kwa ajili ya matatizo ya kifamilia, alikuwa akicheza chini kila timu inapoenda kushambulia.

Akizungumza na Nipashe, Fadlu, alisema anaandaa kikosi chake kwa ajili ya kupata ushindi katika michezo yao inayokuja.

Alisema ni lazima wawe na njia tofauti ya kupata ushindi na si kutegemea aina moja ya uchezaji.

"Tunataka kuhakikisha michezo yetu ijayo tunapata ushindi, tutaanza na huu wa Kombe la Shirikisho na ile ya Ligi, nataka kuona kikosi kinakuwa imara kwenye idara na kutafuta magoli kwa kila namna," alisema Fadlu.

Katika hatua nyingine, Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo amesema kikosi hicho kina wiki nzima sasa kinafanya mazoezi, huku akiweka wazi kuwa wanatarajia kuondoka nchini kati ya Septemba 10-12 kwenda nchini Libya.

"Tutaondoka Septemba kati ya 10, 11, 12 kulingana na upatikanaji wa ndege kwenda kuivaa Al Ahly Tripoli katika mechi yetu ya mkondo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho, hatuna sababu ya kwenda mapema kwa sababu tunajua mazingira ya karibu nchi zote za Afrika, tunajua hata hali za hewa za nchi mbalimbali na mazingira yake, kwa hiyo yale mambo ya kwamba lazima tuwahi ili tuzoee mazingira sisi kwetu hayapo tena," alisema Ahmed.

Aidha, alisema kuwa kikosi hicho kesho kitacheza mchezo mwingine wa kirafiki kwenye Uwanja wa KMC, Mwenge, Dar es Salaam dhidi ya JKT Tanzania.

"Tutacheza mchezo wetu wa kirafiki Jumamosi Uwanja wa KMC Mwenge, Dar es Salaam dhidi ya JKT Tanzania  na ndiyo utakuwa mchezo wetu wa mwisho kabla ya kwenda kuivaa Al Ahly Tripoli.

Mchezo huu wa kirafiki utakuwa na mashabiki, hatuna haja ya kuwakataza mashabiki wetu kuiangalia timu yao, tunawaruhusu waje kwa wingi kuiona Simba yao," alisema Maneja Habari huyo.

Hiyo itakuwa mechi ya pili ya majaribio ya Simba kabla ya kucheza mchezo wao wa kimataifa kwani Jumapili iliyopita ilicheza dhidi ya Al Hilal ya Sudan na kutoka sare ya bao 1-1.