Fadlu akamilisha mkakati kuiua Al Ahly Tripoli

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:33 AM Sep 09 2024
Kocha Mkuu wa miamba hiyo ya Tanzania, Fadlu Davids.
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa miamba hiyo ya Tanzania, Fadlu Davids.

WAKATI kikosi cha Simba kikitarajiwa kuondoka Jumatano usiku kuelekea nchini Libya kwa ajili ya mchezo wa raundi ya kwanza Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Tripoli ya huko, Kocha Mkuu wa miamba hiyo ya Tanzania, Fadlu Davids, amesema kikosi rasmi kiko tayari kwa mashindano.

Juzi katika mchezo wake wa mwisho wa kirafiki, Simba ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam, ambayo yaliwekwa wavuni na Jean Charles Ahoua kwa mkwaju wa penalti na Salehe Karabaka.

Baada ya mchezo huo, kocha Fadlu, alisema mwisho wa mchezo huo unaashiria kuwa sasa wapo tayari kwa mashindano ya kimataifa.

Alisema tayari wachezaji wake wamemaliza ule mzunguko wa wiki sita alizokuwa akihitaji za mazoezi, na mechi ambazo zingewafanya wawe na utimamu wa mwili kwa asilimia 100.

"Kilichobaki ni kuwasoma wapinzani tu, lakini furaha yangu kubwa ni utimamu wa mwili ambao wachezaji wangu wanao, na hii ni tofauti na ilivyokuwa kwenye michezo wa Ngao ya Jamii, ambapo wengi wao hawakuwa nao, pia hawakuwa na pumzi za kucheza kwa dakika zote, lakini sasa zile wiki sita nilizokuwa nazitaka zimekamilika na sasa tupo tayari," alisema Fadlu.

Alisema hana wasiwasi na wachezaji ambao wamekwenda kwenye timu zao za taifa kwa sababu huko nako wanacheza na baadhi yao watajiunga moja kwa moja jijini Tripoli.

Fadlu anaamini mchezo utakaokuwa mgumu kwao ni ule wa ugenini, ambao watatakiwa kucheza kwa juhudi ili kupata matokeo mazuri akiamini kuwa ule wa marudiano ambao utachezwa mbele ya mashabiki wa Simba, utakuwa mzuri kwao.

"Tuna mechi ngumu dhidi ya Al Ahly Tripoli nyumbani kwao, tunacheza mbele ya mashabiki wao ambao najua watawashangilia sana, lakini sisi hivi karibuni tulicheza mechi ya majaribio dhidi ya Al Hilal ya Sudan, imetusaidia sana, ulikuwa ni mchezo mzuri na kipimo tosha kwetu, imetuonesha ambavyo  tupo, najua tukifanya vema ugenini, na sisi tutakuja kucheza mechi ya marudiano mbele ya mashabiki wetu ambao wamekuwa wakitushangilia na kutusapoti sana, tutapata ushindi mbele yao," alisema.

Wakati huo huo, Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema kikosi hicho kitaondoka nchini Jumatano kwenda Tripoli kwa ajili ya mchezo huo utakapigwa Jumapili ijayo, Uwanja wa Juni 11.

"Tutaondoka Jumatano na mchezo wetu utakuwa Jumapili, hatujataka kwenda mapema kwani tunajua mazingira ya karibuni nchi zote za Afrika, tunajua hata hali za hewa za nchini mbalimbali na tabia ya kila nchi tunazijua, kwa hiyo yale mambo ya zamani kwamba lazima tuwahi ili tuzoee mazingira sisi kwetu hayapo tena, sisi ni wenyeji sana katika soka hili," alitamba Ahmed.