HUKU Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, akisema ana matumani makubwa na kikosi hicho kwenye michuano yote ikiwamo Kombe la Shirikisho Afrika na kwamba ni suala la muda tu kabla hawajaanza kuonesha makali yao, amefungua msimu wa Ligi Kuu Bara kwa kuwa mwalimu wa kwanza kutwaa tuzo ya Kocha Bora wa Mwezi Agosti yeye pamoja na Kiungo wa timu hiyo, Jean Charles Ahoua.
Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi jana, imeeleza kuwa Fadlu ametwaa tuzo hiyo kutokana na kuiwezesha Simba kushinda mechi mbili ndani ya mwezi huo baada ya kuichapa Tabora United mabao 3-0 na kisha kupata ushindi wa 4-0 dhidi ya Fountain Gate.
Katika kinyang'anyiro hicho, Fadlu amewashinda Patrick Aussems wa Singida Black Stars na Abdallah Mohamed wa Mashujaa FC.
Kwa upande wa Ahoua ametangazwa kuwa mchezaji bora wa mwezi huo baada ya kuisaidia timu hiyo kuvuna alama hizo saba kwa kufunga bao moja na kuhusika katika mabao mengine matatu.
Kikosi hicho cha Simba, pia Jumamosi iliyopita kilicheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Al Hilal ya Sudan na kutoka sare ya bao 1-1.
Fadlu, alisema taratibu mfumo wake unaanza kuwaingia wachezaji wake na muunganiko aliokuwa akiutaka ameanza kuuona.
Fadlu, alisema bado timu haijafika pale anapopataka, lakini taratibu wanaanza kuonesha kukaribia apatakapo.
"Najua matarajio ya mashabiki wa Simba, najua nini wanakitaka, tunaenda huko, naamini tutafanya vizuri na kurudisha furaha na matumaini yao," alisema Fadlu.
Alisema katika kipindi hiki ambacho ligi imesimama anaendelea kufanyia kazi kile ambacho anakiona bado hakijakaa sawa ndani ya kikosi hicho.
"Natamani kupata tena mchezo wa kirafiki, uwe wa kimataifa au na timu za ndani, kikubwa ni kuangalia kile tunachokifanya mazoezini kimeshikwa na wachezaji, lakini pia itafanya wachezaji wangu waliopo kwenye kikosi kuendelea kuwa kwenye hali ya kushindana tukiwasubiri wale waliopo kwenye vikosi vya timu za taifa," alisema Fadlu.
Katika hatua nyingine, Fadlu amesema amefurahishwa na viwango vya nyota wake Leonel Ateba na golikipa Aishi Manula ambao walicheza kwa mara ya kwanza Jumamosi chini yake.
Kwenye mechi hiyo, Ateba ndiye alikuwa mfungaji wa bao hilo la Simba huku Manula naye akifanya kazi ya ziada kuokoa michomo kadhaa kabla ya kumpisha Hussein Abel ambaye aliruhusu bao kwa wapinzani wao hao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED