Fadlu aanika nafasi tatu za kusajili Simba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:06 AM Dec 31 2024
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, anatarajia kwenda kukaa na viongozi wa klabu hiyo kuangalia nini kifanyike kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi chake.

Akizungumzia tathmini ya kikosi cha timu hiyo baada ya kumalizika kwa michezo 15 ya mzunguko wa kwanza, pamoja na mechi za Kombe la Shirikisho Afrika, kocha huyo raia wa Afrika Kusini, alisema anataka kukaa nao ili waangalie ni mchezaji gani bora anaweza kupatikana kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili wapate kumwongeza kwenye kikosi.

Alisisitiza kuwa hahitaji kuongeza mradi tu ionekana amesajili bali anataka mchezaji ambaye atakuja moja kwa moja kuchukua nafasi au kuleta ushindani mkubwa kwenye kikosi.

"Nakwenda kukaa na viongozi kuangalia nini kifanyike, nani anapatikana sokoni ili tumwongeze, kazi bado ni kubwa, nyuma, katikati na mbele kote kunahitaji maboresho angalau ya mchezaji mmoja mmoja, ukiangalia ushindani kwenye Ligi Kuu ni mkubwa, kuna Azam FC, Singida Black Stars, Tabora United na Yanga pamoja na sisi wote tuna uwezo wa kuchukua ubingwa, hivyo lazima tuendelee kuongeza uimara kwenye kikosi chetu," alisema kocha huyo.

Simba imemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ikiwa kileleni, ikikusanya pointi 40, ikicheza michezo 15, ikishinda 13, sare moja, ikipoteza moja, mabao 31 ya kufunga, ikiruhusu matano.

Akizungumzia michuano ya Kombe la Shirikisho, alisema kundi lao bado ni gumu na kwamba katika makundi yote ndilo unaweza ukaliita la kifo.

“Ninachoweza kusema kundi letu unaweza kuliita kundi la kifo kwa kuwa kila timu ina nafasi ya kufanya kitu tofauti, timu mbili zinatakiwa kusonga mbele, lakini kuna timu tatu au hata nne zina nafasi hiyo, sisi Simba tunatakiwa kuwa na hesabu kubwa kwenye hizi mechi mbili za ugenini na moja ya nyumbani," alisema.

Hata hivyo, alisema wachezaji wake wanatakiwa kubadilika na kutofanya makosa kama waliyoyafanya nchini Algeria walipocheza dhidi ya CS Constantine, akisema ilikuwa ni mechi ya kuondoka na pointi zote tatu, au japo moja, lakini wakapoteza kwa mabao 2-1 kutokana na makosa yao, lakini kwa sasa wamejifunza kutokana makosa hayo.

Kuhusu Elie Mpanzu, winga aliyeanza kuitumikia timu hiyo kipindi cha usajili wa dirisha dogo, alisema yeye binafsi anafurahishwa na kiwango chake ingawa anajua shauku ya mashabiki ni kumuona anafunga mabao au anatengeneza.

"Nimefurahishwa sana na kiwango chake, najua shauku ya mashabiki wa timu hii ni kumuona anafunga bao au anatoa 'asisti', lakini kwangu naona anafanya makubwa uwanjani.

Mimi kama kocha nawaambia wanachama na mashabiki wa Simba, pamoja na wapenzi wa soka watulie hivyo hivyo, atawashangaza sana, kwa sababu nimeshamuona ni mchezaji wa kiwango cha juu sana," alisema Fadlu.