Coastal yawahi Dar kuikaribisha Mashujaa FC

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 09:31 AM Sep 10 2024
Msemaji wa timu hiyo, Abbas el Sabri,
Picha: Mtandao
Msemaji wa timu hiyo, Abbas el Sabri,

KIKOSI cha Coastal Union leo kinatarajia kutua jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao ujao dhidi ya Mashujaa FC utakaopigwa Septemba 13, mwaka huu, katika Uwanja wa KMC uliopo Mwenge, Dar es Salaam.

Akizungumza na Nipashe jana, Msemaji wa timu hiyo, Abbas el Sabri, alisema wachezaji wote wana morali ya juu kuelekea katika mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa mgumu na wenye upinzani mkubwa. 

"Kesho (leo), tutaanza safari kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wetu dhidi ya Mashujaa, ambao tutaucheza kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam, alisema El Sabri.

Alisema wachezaji wote kiafya wanaendelea vizuri na kudai mpaka sasa hakuna mchezaji yeyote ambaye ni majeruhi. 

Aidha, alisema mchezaji wao Lameck Lawi, kwa sasa yupo tayari kucheza na kuweka wazi ataonekana siku hiyo katika mchezo huo.

Aidha, alisema kuwa kwa sasa mchakato wa kumtafuta kocha mkuu bado unaendelea na kwamba zoezi hilo likikamilika watawafahamisha Watanzania wajue kinachoendelea.

"Mchakato wa kutafuta Kocha Mkuu unaendelea vizuri, tukimpata pamoja na wasaidizi wake tutatoa taarifa kwa mashabiki wetu," alisema msemaji huyo.