Chipukizi yashukuru sare kwa Mlandege FC

By Hawa Abdallah , Nipashe
Published at 12:01 PM Sep 09 2024
Kocha Mkuu wa timu ya Chipukizi, Mzee Ali
Picha: Ayoma
Kocha Mkuu wa timu ya Chipukizi, Mzee Ali

TIMU ya Chipukizi FC imesema matokeo ya sare waliyopata dhidi ya Mlandege FC, hayakuwa mabaya hasa kulingana na ugumu uliopo wa michezo hii ya awali ya Ligi Kuu Zanzibar.

Mlandege  FC ililazimishwa sare tasa na Chipukizi FC katika uwanja wake wa nyumbani kwenye mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu Zanzibar uliochezwa  juzi katika Uwanja wa New Amaan Complex.

Akizungumza baada ya kumalizika mchezo huo, Kocha Mkuu wa timu ya Chipukizi, Mzee Ali, alisema timu yake ilikosa utulivu katika dakika zote za mchezo.

Alisema walifanikiwa  kutengeneza nafasi nyingi za wazi, lakini suala la umakini na utulivu ndicho kilichochangia kutopata matokeo ya alama tatu.

Alisema lakini pia kulikuwa na tatizo la kutojiamini kwa wachezaji wake wapya jambo ambalo anadhani ataanza nalo  katika mchezo wake wa pili.

"Kupata sare katika mchezo huu wa kwanza hasa tukiwa ugenini si matokeo mabaya sana, japo tulijiandaa kwa ushindi, tumefanya makosa na tutayafanyia kazi mchezo ujao" alisema.

Naye Kocha Msaidizi wa Mlandege FC, Sabri China, alisema mpaka sasa hafahamu tatizo lilosababisha wachezaji wake kushindwa kupata matokeo chanya.

Alisema wachezaji wake walicheza kwa presha kubwa hali iliyowababishia kushindwa  kufanya majukumu yao vizuri uwanjani.

Alisema makosa yalikuwa mengi katika safu ya ulinzi na ushambuliaji na kusababisha  timu hiyo kushindwa kucheza vizuri hasa katika kuwadhibiti wapinzani wao.

"Hata sijajua tatizo nini, timu haikucheza vizuri kabisa, tunawajua wapinzani wetu mfumo wao ni mashambulizi kwa mpipira mirefu," alisema.

Hata hivyo, alisema watajipanga kuhakikisha wanafanya vizuri  katika mchezo wao wa pili hasa kwa wachezaji wao wapya ambao pia hawakuwa na kiwango kizuri.

Ligi Kuu Zanzibar itaendelea tena leo Jumatatu kwa kupigwa michezo miwili katika viwanja vya Amaan nje 'Annex A' kwa Mafunzo kuvaana na KMKM SC wakati katika Uwanja B, Uhamiaji ikimenyana na Junguni kutoka  Kisiwani Pemba.