Azam kucheza mechi za kirafiki

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 12:34 PM Jan 02 2025
Ofisa Habari wa klabuya Azam FC, Hasheem Ibwe,
Picha: Mtandao
Ofisa Habari wa klabuya Azam FC, Hasheem Ibwe,

UONGOZI wa klabu ya Azam FC umewapa mapumziko mafupi wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo huku wakipanga kucheza michezo kadhaa ya kirafiki pindi watakaporejea kwenye majukumu yao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Hasheem Ibwe, amesema mapumziko waliyopewa wachezaji ni mafupi na wanatarajia kurejea kwenye majukumu yao wiki ijayo.

Alisema mara watakaporudi pamoja na programu za mazoezi pia wanatarajia kucheza michezo miwili mpaka minne ya kirafiki kujiweka sawa kuelekea kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Kwa upande wetu kila kitu kinaenda sawa, wachezaji na benchi la ufundi wapo kwenye mapumziko mafupi, lakini mambo mengine yanaendelea, kocha wetu ametoa programu yake ya mazoezi pindi wachezaji watakaporejea, la zaidi pia kuna michezo ya kirafiki tutacheza kabla ya kurejea kwenye Ligi Kuu," alisema Ibwe.

Aidha, alisema pia wamepokea mialiko kutoka baaadhi ya nchi kwa ajili ya kwenda kucheza michezo ya kimataifa ya kirafiki.

Bila kutaja majina ya klabu, ametaja mialiko hiyo inatoka kwenye nchi za Afrika Kusini, Qatar, zambia na Dubai.

"Uongozi na benchi la ufundi utaangalia kama kuna ulazima wa sisi kwenda huko, kama hawataona ulazima basi tutaendelea na programu ya mwalimu wetu," alisema Ibwe.

Kuhusu dirisha dogo la usajili, Ibwe amesema uongozi umepokea mapendekezo ya mwalimu juu ya wachezaji na kuwaacha na wale wa kuchukuliwa kuongoza nguvu kwenye timu hiyo.

"Taratibu zikishakamilika tutatangaza nani na nani tunaagana nao na nani tutawaongeza, kwa sasa kila kitu kinafanyiwa kazi," alisema Ibwe.

Azam FC inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 36 baada ya kucheza michezo 16 ikizidiwa pointi nne na vinara Simba ambao wamecheza michezo 15.