BAADA ya kutangaza kumsajili beki wa kati raia wa Ivory Coast, Zouzou Landry, klabu ya Azam FC imesema haijamaliza kufanya usajili na wanajiandaa kushusha tena nyota wengine ambao wanahitajika na Kocha Mkuu, Rachid Taoussi.
Mkuu wa Idara wa Habari na Mawasiliano ya Klabu hiyo, Thabit Zacharia, amesema uliofanyika ni usajili wa mwanzo tu kwenye kipindi hiki cha dirisha dogo na watafanya usajili mwingine ili kuendelea kukiboresha kikosi chao.
"Tunasajili kwa maelekezo ya kocha Taoussi, tumemsajili mchezaji huyu na siyo mwisho, hatujamaliza kusajili, tunategemea siku chache zijazo tunatangaza mchezaji mwingine," alisema Zaka Zakazi.
Juzi, klabu hiyo ilitangaza kumsajili, Zouzou, ambaye mbali ya kuwa ni beki wa kati, pia anaweza kucheza beki wa kushoto.
Baada ya kutangazwa kusajiliwa na Azam FC, mchezaji huyo alionyesha kufurahishwa na kuwataka mashabiki wa klabu hiyo kukaa mkao wa kula.
"Ninayo furaha kujiunga na Azam, tutaonana hivi karibuni," alisema mchezaji huyo.
Wakati hayo yakiendelea, wachezaji wa timu hiyo wameanza mazoezi kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
"Tulianza mazoezi tangu Jumatatu kujiandaa na mechi za mzunguko wa pili, tunaendelea hivi na mazoezi, lakini kila baada ya wiki moja tutakuwa tunacheza michezo ya kirafiki.
Nia ni kuangalia jinsi gani tunapiga hatua. Huwezi kufanya tu mazoezi kila siku halafu hujui umefikia wapi, ndiyo maana kocha wetu akasema kuwa anahitaji kufanya mazoezi kila siku na kucheza mechi kila baada ya wiki hadi pale Ligi Kuu itaporejea tena mwezi Machi," alisema Zakazi.
Hadi kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, Azam ipo kwenye nafasi ya tatu kwenye msimamo ikikusanya pointi 36 baada ya kucheza michezo 16 na kushinda michezo 11, sare tatu huku ikipoteza mechi mbili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED