Ateba: Nitafunga sana mabao Simba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:21 PM Sep 03 2024
Straika mpya wa Simba, Leonel Ateba
Picha:Simba
Straika mpya wa Simba, Leonel Ateba

STRAIKA mpya wa Simba, Leonel Ateba, ameahidi kufunga mabao mengi akiwa na klabu hiyo, akiwaambia mashabiki kuwa huu ni msimu wa ushindi na mataji tu, hakuna kingine wanachohitaji.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Ateba, alisema tofauti na watu wengi nchini wanavyomfikiria, kwake kufunga mabao ni jambo ambalo amelizoea, hivyo alishangaa kuona baadhi ya mashabiki wakiwa na wasiwasi naye.

Ateba, alisema kutokana na upendo na ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzake, wakiwa nje na ndani ya uwanja, anaona atapachika mabao mengi na kuvunja rekodi alizoziweka Cameroon akiwa na Dynamo Douala, kabla ya kwenda USM Alger ya Algeria.

"Nimeanza soka langu Tanzania kwa amani na furaha, mechi ya kwanza tu kucheza nimefunga, tena nimefunga dhidi ya timu kubwa, timu ngumu, Al Hilal, nitaendelea kufanya mazoezi kwa bidii, nitaendelea kujituma ili kuweza kushinda mchezo wetu wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Tripoli, kwenye mchezo huo nitakuwa vizuri zaidi ya mashabiki walivyoniona katika mechi dhidi ya Al Hilal na tutafanya vema," alisema straika huyo aliyesajiliwa badala ya raia wa Ivory Coast, Freddy Michael.

Ateba, amewaahidi wanachama na mashabiki wa timu hiyo, kufunga mabao mengi zaidi, kwani ndiyo kazi yake iliyomteta Tanzania.

"Naahidi nitaendelea kufunga mabao mengi zaidi na zaidi nikiwa na Klabu ya Simba, najua mpira si mchezo rahisi, lakini nimekuja hapa kutafuta matokeo, ninakuwa na furaha nikifunga bao, lakini kama Simba ikishinda mechi nitakuwa na furaha zaidi, ninachowaambia mashabiki wa Simba ni kwamba waje kwa wingi uwanjani kila tunapocheza kutushangilia, msimu huu tunataka kushinda tu, pamoja na kutwaa mataji, hakuna kingine," alisema straika huyo.

Ateba, ambaye alisubiriwa kwa hamu na wanachama na mashabiki tangu katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tabora United na wa pili dhidi ya Fountain Gate na kushindwa kuonekana kwa sababu za vibali, alionekana kwa mara ya kwanza katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Al Hilal ya Sudan, Jumapili iliyopita.

Katika mchezo huo, aliwapa zawadi ya bao dakika ya 26, ambalo liliifanya timu hiyo kutoka sare ya bao 1-1, mchezo uliochezwa, Uwanja wa KMC uliopo Mwenge, Dar es Salaam.

Wakati huo huo, klabu hiyo imesema itakuwa na mchezo mwingine wa kirafiki, Jumamosi ijayo.

Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema kuwa mchezo huo ni moja kati ya mapendelezo ya kocha Faldu Davids katika kukinoa kikosi kabla ya mchezo wake dhidi ya Al Ahly Tripoli.

Hata hivyo, hakuitaja timu watakayocheza nayo wala uwanja, akisema mambo yatakapokaa sawa, ataweka kila kitu hadharani.