Ahoua hatari mabao mguu wa kulia Ligi Kuu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:15 AM Jan 11 2025
KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Jean Ahoua.
Picha: Mtandao
KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Jean Ahoua.

KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Jean Ahoua, anaongoza kwa kupachika mabao kutumia mguu wa kulia kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo kwa sasa iko mapumzikoni hadi Machi mwaka huu.

Kwa mujibu wa dawati letu la takwimu za michezo, Ahoua, amepachika mabao saba kwenye Ligi Kuu mpaka sasa kwa kutumia mguu wa kulia.

Hiyo ina maana mabao yote saba ambayo ameyafunga mpaka sasa kwenye ligi, ameyapachika kwa kutumia mguu huo.

Mchezaji huyo raia wa Ivory Coast aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu huu kutoka klabu ya Stella d'Adjame, amepachika mabao saba kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa nyuma ya kinara wa mabao, Elvis Rupia, raia wa Kenya anayeichezea, Singida Black Stars ambaye amefunga mabao manane.

Mastraika wawili, Clement Mzize wa Yanga na Selemani Mwalimu wa Fountain Gate, wamefunga mabao matano kila mmoja kwa kutumia mguu huo.

Hata hivyo, wachezaji wote hao wamepachika mabao sita kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka kumalizika kwa mzunguko wa kwanza.

Jumla ya wachezaji sita wanakamata nafasi ya tatu kwa kufunga mabao kwa mguu wa kulia.

Wachezaji hao ni Edger William wa Fountain Gate, Elvis Rupia wa Singida Black Stars, Paul Peter wa Dodoma Jiji, Idd Selemani 'Nado' na Feisal Salum, wote wa Azam FC, na Marouf Tchakei ambaye mzunguko wa kwanza aliichezea Tabora United kwa mkopo na sasa amerejea kwenye klabu yake ya awali ya Singida Black Stars.

Hadi kumalizika kwa mzunguko kwanza, jumla ya mabao 264 yamefungwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo imemaliza mzunguko wa kwanza huku baadhi ya timu zikiwa zimeshacheza mechi za kwanza za mzunguko wa pili.

Takwimu zinaonyesha kuwa mabao hayo yamefungwa kwenye michezo 127 iliyochezwa mpaka sasa.

Katika michezo hiyo, mechi 94 zimetoa washindi na 33 zimeishia kwa sare.

Katika michezo 94 ambayo timu zimeshinda, mechi 58 timu zimepatia ushindi zikicheza nyumbani na mechi 36 zimetoa washindi wakicheza ugenini.