WAENDESHA baiskeli nane kutoka Naironi nchini Kenya, wametumia siku nne kufika mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kukabidhi wanafunzi mabegi maalum ya shule yaliyotengenezwa kwa plastiki.
Mabegi hayo yamegawiwa kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro mkoani humo.
Akizungumza wakati wa kuwapokea waendesha baiskeli hao pamoja na kugawa mabegi hayo, Meneja wa KLM kwa upande wa Tanzania, Rajat Kumar, alisema mpango huo wa kutengeneza mabegi ya plastiki ni mkakati wao wa kutunza mazingira.
Alisema mabegi hayo yametengenezwa kutokana na chupa za plastiki zilizotumika kwenye ndege za shirika hilo.
"Waendesha baiskeli hawa ambao wametumia siku nne kutoka Nairobi kuja Kilimanjaro wanaungana na jamii nyingine katika mkakati wa kutunza mazingira kama tunavyopambania KLM," alisema Kumar.
Alisema Tanzania ni nchi ya pili kupokea mabegi hayo kwa nchi za Afrika na kwamba ya kwanza ilikuwa Kenya ambapo mabegi hayo yalipokewa kwa shule ya Msingi Muthangari jijini Nairobi, Februari mwaka huu.
Waendesha baiskeli hao wanatarajia kuanza safari ya kurejea Nairobi baada ya kufanikisha safari hiyo maalum.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED