MUHAS yahimiza jamii kuishi kiafya kupitia michezo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:24 PM Feb 07 2026
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof. Appolinary Kamuhabwa, (mwenye kofia ya bluu,)warmsup baada ya kushiriki mbio za kilomita 10 za Reunion Fun Run Msimu wa 4, zilizoandaliwa na Chuo hicho jijini Dar es Salaam

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Appolinary Kamuhabwa, amesema chuo hicho kimeendelea kuimarisha mshikamano wa wahitimu wake na jamii kwa ujumla kupitia shughuli za michezo, matembezi na mbio za marathon zinazofanyika mara moja kila mwaka.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof. Appolinary Kamuhabwa, (mwenye kofia ya bluu,)warmsup baada ya kushiriki mbio za kilomita 10 za Reunion Fun Run Msimu wa 4, zilizoandaliwa na Chuo hicho jijini Dar es Salaam leo.Profesa Kamuhabwa amesema mpango huo unalenga kuwakutanisha wahitimu waliomaliza masomo yao katika nyakati tofauti na wanaofanya kazi maeneo mbalimbali, ili warejee chuoni kama nyumbani, kubadilishana mawazo na kuchangia maendeleo ya MUHAS pamoja na ustawi wa jamii.

Ameeleza kuwa MUHAS pia imeanzisha mfumo wa kidijitali unaowaunganisha wahitimu kupitia majukwaa mbalimbali ya mtandaoni, ikiwemo tovuti rasmi ya chuo na makundi ya WhatsApp kulingana na fani au mwaka wa kuhitimu, hatua inayorahisisha mawasiliano na kuimarisha ushirikiano.

“Kwa mara ya nne sasa tunafanya tukio hili na mwitikio umekuwa mkubwa. Mwaka huu zaidi ya wahitimu 500 wamejisajili kushiriki. Hii inatusaidia kupanga mikakati ya kuendeleza chuo na mchango wake kwa jamii,” amesema Profesa Kamuhabwa.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa mazoezi ya mwili katika kuzuia magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari na shinikizo la damu, akibainisha kuwa MUHAS kama chuo cha afya kina wajibu wa kuwa mfano bora kwa jamii katika kuhamasisha maisha yenye afya.

Katika hatua nyingine, Profesa Kamuhabwa amesema MUHAS imeanzisha mfuko wa hisani uitwao Ali Hassan Mwinyi MUHAS Endowment Trust Fund, kwa lengo la kuenzi mchango wa Mkuu wa kwanza wa chuo hicho, Hayati Ali Hassan Mwinyi, na kusaidia maendeleo ya taasisi ikiwemo ujenzi wa mabweni, uboreshaji wa miundombinu na kuwasaidia wanafunzi wenye uhitaji.

Ameongeza kuwa chuo hicho kinaendelea kuvutia wanafunzi wa kigeni kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Marekani, Ujerumani, Australia na Sweden, wengi wao wakija kwa mafunzo ya muda mfupi baada ya kupata taarifa kuhusu MUHAS kupitia tovuti na mitandao ya kijamii ya chuo.

Kwa sasa, wanafunzi wa kigeni wanachangia takribani asilimia 10 ya udahili wote, huku chuo kikilenga kufikia kati ya asilimia 15 hadi 30 katika miaka ijayo, sambamba na upanuzi wa miundombinu na ongezeko la watumishi kufuatia vibali vipya vya ajira vilivyotolewa na Serikali.

Akizungumza kwa niaba ya waandaaji, Mhadhiri Mwandamizi wa Afya ya Jamii na Mkuu wa Kitengo cha Umataifaifishaji na Convocation MUHAS, Mariam Amour, amesema tukio hilo lijulikanalo kama MUHAS Fun Run Season 4 limefanyika kwa mwaka wa nne mfululizo na linaendelea kukua kila mwaka.

Amesema mwaka huu zaidi ya watu 500 wameshiriki, ikilinganishwa na takribani washiriki 200 katika mwaka wa kwanza, huku fedha zilizokusanywa zikielekezwa kwenye mfuko wa Ali Hassan Mwinyi MUHAS Trust Fund kwa ajili ya kusaidia ufundishaji, tafiti, miundombinu na ufadhili wa wanafunzi.

Kwa upande wake, Rais wa Jumuiya ya Wahitimu wa MUHAS, Marsha Macatta Yambi, amesema tukio hilo limevuka malengo yaliyowekwa kutokana na idadi kubwa ya washiriki, hali inayoonesha mshikamano, uzalendo na dhamira ya wahitimu kuchangia maendeleo ya chuo na ustawi wa jamii.

Ametoa wito kwa wahitimu wengine na wadau wa afya kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za MUHAS kama njia ya kuimarisha elimu, afya na maendeleo endelevu ya jamii kwa ujumla.