Benki ya CRDB yazindua michuano Supa Cup 2024

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:54 AM Sep 04 2024
Wafanyakazi wa Benki ya CRDB wakipambana katika mchezo wa netiboli katika michuano ya CRDB Bank Supa Cup 2024, inayoendelea jijini Dodoma.
MPIGAPICHA WETU
Wafanyakazi wa Benki ya CRDB wakipambana katika mchezo wa netiboli katika michuano ya CRDB Bank Supa Cup 2024, inayoendelea jijini Dodoma.

BENKI ya CRDB imezindua rasmi msimu mpya wa mashindano ya soka na netiboli yajulikanayo kwa jina la CRDB Bank Supa Cup 2024.

Uzinduzi huo umefanyika jijini Dodoma jana katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya John Merlin, ukiongozwa na Mkuu wa Fedha wa benki hiyo, Fredrick Nshekanabo, pamoja na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Godfrey Rutasingwa.

Akizungumza katika hafla ya  uzinduzi, Nshekanabo alisema lengo kuu la mashindano hayo ni kuongeza ari, nguvu na ushirikiano baina ya wafanyakazi wa benki.

“Baada ya kusambaza tabasamu kwa wananchi wa Tanzania na kuvuka mipaka ya nchi na kwenda nchini DR Congo na Burundi, sasa ni zamu ya tabasamu hilo kurudi nyumbani kwa wafanyakazi,” alisema Nshekanabo.

Alisema kuwa mashindano hayo yatashirikisha wafanyakazi wa Benki ya CRDB kutoka matawi mbalimbali, pamoja na makao makuu wakishindana vilivyo kugombania kombe la msimu.

Aidha, mashindano hayo yalienda sambasamba na programu ya kujitolea kwa wafanyakazi wa benki hiyo wakiongozwa na Mkurugeni wa Rasilimali Watu kutoa misaada ya vifaa vya kazi katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, kuchangia damu, pamoja na kutoa chakula na vinywaji kwa wagonjwa hospitalini hapo.

Benki ya CRDB ilianzia programu hiyo maalumu ya wafanyakazi wake kujitolea mwaka huu ikilenga kusogea karibu kwa jamii wanayoihudumia. 

Kwa upande wa Rutasingwa, alisema benki yao ni sehemu ya Jamii na ndiyo maana wamekuwa mara kwa mara wakishiriki katika program za kusaidia jamii.

“Sisi kama Benki ya CRDB ni sehemu ya jamii na hatuna budi kurudi kwao kuchangia chochote kile ili kusogeza mbele maendeleo yetu. 

"Programu hii ilizinduliwa visiwani Zanzibar mwezi uliopita na tunatarajia kuendelea kufanya hivyo katika mikoa mingine baada ya hapa Dodoma," alisema.