Uwekezaji kurudisha miti asili nyenzo inayobadili maisha ya watu na vijiji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:36 PM Aug 02 2024
news
PICHA:MTANDAO
Mazingira asili ya Udizungwa.

WIZARA ya Maliasili na Utalii, inatahadharisha kuwa kila mwaka zaidi ya hekta 400,000 za miti ya asili zinapotea zikikatwa kupata ardhi ya kujenga au kulima, mbao, kuni na mkaa.

Kukata miti hiyo muhimu inayopunguza athari za mabadiliko ya tabianchi si jambo jema kwani ni kuondoa ‘mapafu’ yanayofyonza hewa ukaa na kupunguza joto duniani. 

Lakini jambo kubwa ni nani anayerudisha miti hiyo mamilioni inayokatwa kila uchao? Juhudi za kunusuru isikatwe zaidi zinachukuliwa na wadau wanaookoa mazingira, ikiwamo kampuni Udizungwa Corridor Limited inayoendeleza kazi hiyo wilayani Kilolo mkoani Iringa. 

Uongozi wa kampuni hiyo umeingia makubaliano na vijiji vya Itonya, Mhanga na Uluti ili kuzuia ukataji miti hovyo wakati miti mipya inapopandwa. 

Katika makubaliano hayo wananchi ndiyo wanaopanda miti na kusimamia ukuaji wake kwa lengo la kuendeleza maisha ya bayoanuai zote watu, wanyama na mimea.
 Hans Kadinda (22) anayeishi kijiji cha  Itonya wilaya ya Kilolo ni mwenye matumaini ya kuwa uwekezaji huo unalinda mazingira na kuboresha maisha ya  wengine  na ataweza kuwa na maisha bora kwake na mkewe na  mtoto wao.

Akiwa mmoja wa wafanyakazi 150  wa kampuni ya Udizungwa Corridor, tangu mwaka 2021, anasema kuwa na kesho iliyobora ni hakika kwa upande wake kwa sababu uwekezaji kwenye miti umeangalia pia maisha bora kwa vijana na wanavijiji.

 Japo hakuendelea na masomo ya sekondari kutokana na hali duni ya familia , Kadinda anajiunga na akifanyakazi ya upishi katika kambi ya kampuni hiyo  iliyopo kijijini Mhanga inayo jishughulisha na kupanda miti.

 Pamoja na kazi hiyo anamiliki pikipiki na amemfungulia duka mzazi mwenzake kijijini Mhanga ili kumwezesha  kimapato.

Kadinda ni mmoja ya vijana wazawa wa wilaya ya Kilolo ambao wameajiriwa na UCL kampuni ambayo imewekeza kwenye mradi wa kupanda miti ya asili katika milima ya Udizungwa. 

Miti mingi ya asili katika milima hiyo iliyopo kwenye ukanda wa Tao la Mshariki ilikatwa na wanavijiji na hata wageni kwa ajili ya matumizi mbalimbali na kama wataalamu wa msitu wanavyosema kila mwaka  zaidi ya hekta 400,000 za miti ya asili hukatwa nayo pia ilitumbukia kwenye janga hilo. 

Mtendaji wa kijiji cha Uluti, Zainabu Usama, anasema ujio wa kampuni hiyo umezuia ukataji haramu wa miti ya asili kutengeneza mkaa, mbao na kuni kwa matumizi ya nyumbani. 

Anaongeza kuwa pamoja na ajira zilizopatikana, kijiji chake pia kimeweza kushuhudia biashara nyingi kama bodaboda, maduka na minada zikiongezeka kutokana na ongezeko la mzunguko wa pesa. 

"Malipo ikiwamo  mishahara, inaongeza mzunguko wa fedha kwenye  minada na biashara nyingine . Vitu mbalimbali vinanunuliwa katika kijiji cha Mhanga kwenye ofisi na kambi ya UCL  na pote kwenye kuuza na kununua.” Anasema. 

Zainabu anasema wafanyabiashara wanatoka sehemu mbalimbali kama vile makao makuu ya wilaya Kilolo kuja kuuza bidhaa zao na yote yamekuza biashara na uwekezaji.

Mtendaji huyo wa kijiji ambaye ni msomi wa chuo kikuu huria, anasema uwepo wa shughuli za kupanda miti  unakinufaisha kijiji hicho kwani kinapokea  Sh. milioni 10 kila mwaka kama fidia ya kutunza misitu asilia inayonyonya hewa ukaa.
 Mwenyekiti wa Kijiji cha Uluti, Aidan Mmewa anaungana na Zainabu akiongeza kwamba tangu mwaka 2021, kumekuwepo na ongezeko la maendeleo  mfano nyumba za bati kijijini hapo zimeongezeka.

Mumewe anasema  ongezeko la watu katika kijiji hicho kunatokana na wafanyakazi na vibarua wa UCL umechochea  mzunguko wa pesa katika eneo hilo.
 "Vijana wetu wanapata kipato kutokana na uwepo wa ongezeko la watu wanaofanya kazi ya kupanda na kutunza miti ya asili," anasema.

Anasema pamoja na kupokea mrahaba wa kutunza miti, kampuni hiyo inachangia maendeleo mfano, kukamilisha majengo ya shule ya sekondari, vyoo vya Shule ya Msingi Mhanga na ofisi za kijiji chake.

 Akizungumzia mafanikio ya kampuni ya Udzungwa,  kwa kushirikiana na vijiji kadhaa wilayani Kilolo, Mkurugenzi Mkuu  Fredrick Jailosi, anasema wameajiri zaidi ya wafanyakazi 150 na vibarua wengine wengi wanaofanya kazi kwa msimu kila mwaka.
 "Wakati wa msimu wa kupanda miti kati ya mwezi Januari na Machi tunakuwa na vibarua zaidi ya 1,000  wanaofanya kazi kwa miezi sita kila mwaka," anasema Jailos.

Anaongeza kuwa  kampuni inavilipa vijiji vinavyomiliki ardhi inayopandwa miti  Shilingi 35,570 ambayo ni kodi ya pango kwa kila ekari moja kwa mwaka.
 "Ardhi tunayolipia ni ile ambayo imeachwa baada ya kukatwa miti na sasa haina ubora wala thamani ya kufanya kilimo," anasema mkurugenzi huyo.

Anafafanua kuwa kampuni hiyo inayomilikiwa na Tanzania Forest Conservation Group na wakulima wadogo 174, ina malengo ya kupanda miti ya asili katika eneo la ekari 18,000.
 Jailos anasema aina mbalimbali zaidi ya 100 za miti ya asili itapandwa wilayani humo kwa uwekezaji wa zaidi ya Sh. bilioni 90.  

Alisema uwekezaji huo ambao ni wa muda mrefu mpaka mwaka 2051, unatarajiwa kuingiza mapato kupitia biashara ya hewa ukaa.

 Mapato yatakayopatikana yatagawanya kwa ulinganifu  yaani asilimia 50 kila mmoja kwa TFCG na wakulima wadogo ambao ni wanahisa. 

"Lakini vijiji vitaendelea kupata malipo ya kila mwaka kama pango la ardhi na gharama za kutokata miti," mkurugenzi huyo anasisitiza.

 Pango la ardhi la kila mwaka linatarajiwa kuongezeka kutoka 35,570 kwa ekari mwaka 2022 mpaka 68,000 itakapofika mwaka 2051 huku malipo ya hewa ukaa yatafikia  bilioni  8.7 kwa mwaka.

Anasema vijiji pia vitapata malipo ya mavuno ya miti kwa ajili ya mbao na matumizi mengine kwa mujibu wa mkataba baina yao na mwekezaji.