Mtatiro: Huyu ndiye Rais wa TLS tumtakaye

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 03:44 PM Jul 31 2024
Wakili Julius Mtatiro.
Picha: Nipashe Digital
Wakili Julius Mtatiro.

MKUU wa Wilaya ya Shinyanga, na Mwanataaluma ya Sheria, Wakili Julius Mtatiro amewachambua wagombea urais TLS na kutoa maoni yake.

"Watanzania na Mawakili tumesikiliza na kufuatilia kwa kina, mjadala wa wazi uliorushwa na Star TV Julai 27 mwaka huu ukiwahusisha mawakili mbalimbali waliopendekezwa kuwania nafasi ya juu ya urais  wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

"Sisi ambao tuko kwenye tasnia ya sheria, kwa muda mrefu tumepata wasaa wa kutosha wa kuwafuatilia wagombea mbalimbali wa nafasi husika, kwa sababu wamekuwa ni wenzetu kwa 
namna moja au nyingine.

"Tunawapongeza sana mawakili wote walioshiriki katika mjadala huo wa wazi na ambao wanaendelea na kampeni na tunawatakia kila la heri,"anasema Mtatiro.

Mwanataluma huyo, anasema wao  amepata wazo la umuhimu wa kufanya uchambuzi kwa wagombea hao ili kuongeza na kushajiisha mjadala unaoweza kusababisha TLS ikaendelea 
kupata viongozi bora watakaoendeleza kazi nzuri  kwa mujibu wa sheria inayounda chama hicho.

"Kipekee na kwa nia njema, tumeona tuelekeze uchambuzi wetu kwa wagombea ambao tunadhani wanaweza kuweka ushindani wa kipekee katika kinyang’anyiro cha urais wa TLS.Hii ni kwa sababu, licha ya kuwa tunatambua umuhimu wa wagombea wote, lakini tunatumia uhuru wetu wa kichambuzi kuona shabaha ya mielekeo halisi ya nani na nani wanaonekana wana nguvu dhahiri katika kinyang’anyiro hiki na wana nafasi ya kukwea katika nafasi ya juu kuliko wengine," anasema Mtatiro.

"Wengi wetu tumejifunza kuwa, wagombea wote sita waliofuzu ni wazoefu na wana sifa mbalimbaliza kiuongozi.Kila mmoja ana sifa za kipekee tofauti na wenzake na kila mmoja akiwa na uzoefu wa kipekee ambao si lazima ufanane na mwingine, na kwa hiyo ni wazi kuwa kila mgombea anaweza kuleta mabadiliko fulani au matatizo fulani atakavyopata nafasi ya kuhudumu urais wa TLS."

Alisema kabla ya kufanya uchambuzi huo walikuwa na maswali mbalimbali vichwani mwao kuhusiana na  TLS na aina ya  rais inayemhitaji kwa muktadha wa sasa wa nchi.

"Ni wazi kwamba, TLS kwa sasa kinahitaji rais ambaye haji kujianzishia tu mambo yake vile atakavyo, kinahitaji rais ambaye atakuja kuendeleza na kuweka mkazo kwenye mambo muhimu na mazuri (misingi)iliyowekwa na watangulizi wake ambao wamefanya majukumu yao na kurekebisha maeneo ambayo hayakufanyika vizuri, bila kusahau kujenga uwezo wa kuwaunganisha mawakili,"anasema Mtatiro.

"TLS ni Chama cha kitaaluma kinahitaji rais mtendaji, mweledi, mtulivu, mwenye uwezo wa ushawishi wadau wote wa sheria ndani ya nchi, mwenye maono yanayoweza kutekelezeka bila 
papara. 

"Atakayeweza kuwaunganisha mawakili wote, kiungo muhimu kati ya TLS na mdau mkuu ambaye ni serikali,na ambaye hatogeuka kuwa msanii na mpiga kelele, kueneza chuki kwa misingi ya uanaharakati, utofauti wa ufuasi wa vyama vya siasa, mihemko na jazba.

TLS inahitaji mtu mwenye visheni na busara za kutosha, ambaye anaweza kukisaidia chama kutekeleza majukumu yake katika hali ya utulivu na ufanyaji maamuzi wa pamoja na wenye tija."