HERI ya sikukuu ya Noeli pamoja ujio wa mwaka mpya. Ni safari za kurudi nyumbani, ukitembelea mitandao ya ‘booking’ na ukifika vituo vya mabasi unaelezwa kila kitu kimejaa. Watu wanatoka mijini na majiji kwenda vijijini kusherehekea Krismasi, kumaliza mwaka na kuanza mwaka mpya 2025.
Lakini kikubwa ni kutambua kuwa ukitumia pesa nyingi vibaya tena ulizokopa benki, au kwa wakausha damu, ama ndugu au kuweka mali zako rehani kutangaza ufalme vijijini au popote kwa ndugu zako unajidanganya na Krismas na mwaka mpya vitakufundisha adabu au kukutokea puani.
Ni wakati wa kuwa na nidhamu ya fedha na kuacha kununua vitu vingi usivyohitaji na kulewa au kunywa kupindukia, kununua ng’ombe, mbuzi na kuku ukiwafurahisha marafiki kwa lengo la kujitutumua na kutangaza ufalme au usharobaro.
Kuna wengine ili aonekane ni 'kibosile', anaingia kijijini au popote akiendesha magari ya kifahari lakini ya kukodi au kuazima. Ni jambo jema kufanya kile roho inapenda lakini hilo halifai kujifanya mmiliki wa Ford Ranger, Jeep au Hammer ambayo si yako ili marafiki, wanawake na wananchi wakuone uko vizuri kumbe njaa kali.
Kumbukeni kuwa sherehe zinapomalizika unaanza kilio, msongo wa mawazo, maradhi ya afya ya akili baada ya kuwa na wakati mgumu kutokana na kushindwa kulipa madeni makubwa uliyojisababishia kuanzia kukodi magari na mikopo ya fedha za watu uliyochukua.
Utalia zaidi ukishindwa kuwalipia watoto na wategemezi wako ada ya Januari ambayo inaambatana na vifaa vya shule kama sare, magodoro kwa wanaokwenda bweni.
La muhimu sherehe hizi zisiwe za kuendeleza ubadhirifu na matumizi mabaya ya miili yenu kuanzia ngono, ulevi kupindukia, kula mno ambavyo huwaacha watu wengi na uchungu, sonona, shida ya akili baada ya kuchezea fedha kiholela bila sababu na kunufaisha wafanyabiashara mijini na vijijini.
Kuna madai kuwa huu ndio msimu wa ngono. Hilo nalo mabinti na wanafunzi wajiangalie wasijiachie wakawa wameambukizwa maradhi na kupata mimba wakashindwa kusoma Januari 2025.
Baadhi ya wafanyabiashara wa chakula, pombe na nyumba za wageni Manzese jijini Dar es Salaam wanasema msimu wa sherehe hizo ndizo nyakati za kupata fedha kwa sababu ni kama “watu hupata wazimu”. Matumizi makubwa ya pombe, chakula na nyumba za kulala wageni yanaongezeka kuliko kawaida.
Wanaiambia Nipashe kuwa wanapata fedha maradufu na mara nyingi malengo ya mauzo wakati huu wa sikukuu ni makubwa na pesa zinapatikana vyakutosha.
Watu wanatumia milioni kadhaa kuanzia mkesha wa Krismasi, hadi mwaka mpya, lakini baada ya hapo wanaanza kuomba mkopo kwa jamaa zao wa vijijini au marafiki hata kuweka mali rehani ili waweze kurudi kazini mijini na kutatua shida zao za kifedha.
Kumbuka ulevi na sherehe husababisha ajali, kuua, kujeruhi na kukamatwa, ukashtakiwa kwa kusababisha yote hayo kisa kuendesha gari kiholela. Kuna uwezekano wa kuishi rumande kwa siku kadhaa maana hakuna anayeweza kukudhamini kwa ujanja na starehe zako.
Usisahau pia kuna uwezekano wa kufukuzwa kwa sababu ya mambo kama hayo ya utovu wa nidhamu. Wakati huna kazi ndio muda wa kampuni za kukodisha magari zitadai fedha zake na wale uliochukua mikopo watakukalia kooni.
Kumbuke ni heri kufunga na kuomba kuliko kujifurahisha kwenye karamu za aina hiyo zinazokuharibia mipango na kuendeleza ulafi. Tena kwenye sherehe hizo ndio wakati wa kusikia taarifa za uharibifu wa mali kuumizana kwenye pombe na kupoteza vitu vya thamani.
Usipoangalia unaweza kuuza mali kama nyumba na mashamba kufidia mali za watu hasa fedha na magari ulizokopa au kuharibu.
Aidha, Desemba ndio ambao kukopesha pesa kunanoga, wazee wa kausha damu wanakuwa kazini kwao ni mwezi wa 'kumeki’ na kupata faida, anadokeza mjasiriamali anayetoa mikopo eneo la Mwenge Dar es Salaam.
“Wanaofanya biashara hii ya kukopesha fedha hawana tatizo na wazee wa matumizi wanachotafuta kwako ni fedha zako tu. Lazima uweke dhamana nono wewe mteja wetu na kupewa riba kubwa ili usipotimiza ahadi wajue namna ya kukukamua au kukukausha damu.” Anasema jina lake na kampuni tunalitunza kuheshimu wateja wake.
Anaongeza “Hawaangalii wanaacha laptop, simu za thamani, vito hasa dhahabu na tanzanite, nguo za bei ghali na wengine samani. Sisi hatuna shida…” anasema.
Kumbukeni ukosefu wa nidhamu ya pesa ndicho chanzo cha mambo hayo ambayo wengi hayawasaidii.
TAHADHARI MVUA
Kuna taarifa za mvua kubwa wilayani Same mkoani Kilimanjaro na pia mikoa ya Rukwa na Katavi, hivyo watu wanaposherehekea siku kuu wasisahau taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA).
Ni vyema kuchukua tahadhari ya mvua wakati wa sikukuu katika maeneo mbalimbali usijisahau mafuriko na vimbunga havijua Krismas tena havina mwaka mpya.
Mvua kubwa zinaambatana na ngurumo na radi, hivyo wakazi katika maeneo yenye mvua za vuli wawe macho kwa kuwa ajali zinaweza kutokea na kuwa misiba badala ya sherehe.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED