MAREKEBISHO SHERIA YA NDOA; Watetezi wamshangaa waziri kuendeleza mfumo dume

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:02 AM Nov 27 2024
Mwanaharakati Dk. Ananilea Nkya
Picha Zote: Mtandao
Mwanaharakati Dk. Ananilea Nkya

BAADA ya Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, kueleza kuwa kifungu kilichotumika katika kesi ya kubadilisha Sheria ya Ndoa ya 1971, siyo sahihi, wanaharakati wamshangaa kuendeleza mfumo dume.

Kesi ya kupinga umri wa ndoa, ilifunguliwa na Shirika la Msichana Initiative, ilipata ushindi kwenye mahakama ya rufani iliyoamuru vifungu 13 na 17 ambavyo vinaruhusu binti wa miaka 14 au 15 kuolewa, vifutwe.

Akichambua maelezo ya Waziri Kabudi, mwanasheria nguli na mtetezi wa haki za binadamu, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, anasema mahakama ndiyo iliyotakiwa kusema kifungu hicho si sahihi na si mwingine.

Anaeleza kuwa kifungu cha 13 na 17 cha Sheria ya Ndoa ya 1971, kinafahamika na Mahakama ya Rufani na ndiyo iliyoelekeza kukifuta kama ingekuwa si sahihi isingefanya hivyo kwani ilikiona na kusikiliza hoja na kutoa maamuzi.

“Serikali iache visingizio na kuamua kwamba si sahihi mtoto chini ya miaka 15 kuolewa,” anasema Dk. Hellen mwasisi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu-LHRC.

Wazo analosema Waziri Kabudi ni maoni yake kwa sababu kama ingekuwa hivyo, mahakama ilitakiwa itoe maoni hayo lakini imeona upungufu wa kisheria, hivyo wanatakiwa wakiondoe na si kupingana na chombo cha juu cha kutafsiri sheria na kulinda haki.

“Profesa Kabudi ni mwalimu wa sheria, kwenye familia ana msimamo kuwa tusome na tuangalie mambo ya anthropolojia ya sheria na tuunganishe na masuala ya jamii. Hili si suala la kijamii pekee , kwa sababu tiba za kisasa na utafiti, unaonesha kwamba mtoto akiolewa anaathirika na mengi,” anasema Dk. Hellen.

Anthropolojia ni elimu inayochunguza maisha ya binadamu kwenye historia, ndani  ya jamii, utamaduni, taratibu na  hatua alizopitia na anazoendelea nazo hata sasa.

Anataja vifo vya mama na mtoto, fistula, matatizo ya afya ya akili, ulemavu wa nyonga na maradhi yasiyotibika kama saratani ya kizazi kuwa ni baadhi ya athari.

Anasema sheria haipaswi kuangalia anthrolopojia na jamii, bali pia masuala ya afya na maisha ya binti anayeingia kwenye ndoa akiwa na umri mdogo.

Anasisitiza kwamba sheria irekebishwe kama hukumu ya Mahakama ya Rufani ilivyoelekeza, ili kuwa na jamii yenye afya timamu ya akili na mwili.

Mwanaharakati Dk. Ananilea Nkya, akizungumzia majibu ya Profesa Kabudi, kuhusu marekebisho ya sheria ya ndoa na hukumu ya Mahakama ya Rufani, anasema ameendelea kutetea mfumo dume unaowaminya haki watoto wa kike.

Anasema wakati mwingine kauli za viongozi kama hizo, zinawafanya wananchi waamini kuwa wanaosimamia watoto wao hawajali hatima zao, kwa sababu wanafamilia wa viongozi kama hao hawataathirika na ndoa au mimba za utotoni.

Anapinga maelezo ya Waziri Kabudi kwamba kulitakiwa kuwe na vifungu vya maelezo, maoni (commentary) kwenye katiba, akieleza kuwa kuna sheria zimerekebishwa ikiwamo ya mtoto ya 2009 ambayo haikugusa katiba.

Anamkumbusha Profesa Kabudi kuwa Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (1998) inayoharamisha pamoja na mambo mengine, ukeketaji na matendo ya ngono kwa watoto, ubakaji na ulawiti, na kutoa hukumu ya zaidi ya miaka 30 au maisha kwa wanaopatikana na hatia.

“Akumbuke ziliandikwa bila kuwekwa maoni ya kikatiba anayoyazungumzia. Ni mwanasheria na Waziri, mbona hazungumzii sheria ya uchaguzi na katiba inayokataza watoto wenye miaka 13 kupiga kura? Lakini mbona hawapewi mikopo benki? Inakuwaje waruhusiwe kuolewa?” Anahoji Ananilea.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, anasema kuendeleza mjadala ya kupinga marekebisho ya vifungu hivyo, kunaleta wasiwasi kwamba mfumo hauko tayari kuwalinda mabinti kwa kisingizio cha kusubiri marekebisho ya katiba.

Anasema huenda waziri hakubali mabadiliko kwa sababu ana uhakika watoto na wajukuu zake hawawezi kuingia kwenye ndoa hizo.

Anafafanua kuwa ndoa hizo ni matatizo yanayowapata watoto wa raia maskini, wasio na ufahamu na elimu, walio duni kiuchumi, wanaosoma shule za mbali, zisizo na mabweni, wala chakula na jamii inayowazunguka inanyanyasa watoto na kuendeleza mfumo dume na mila kandamizi, jambo ambalo halihusu familia za viongozi.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa, akikosoa maoni ya Waziri Kabudi, anaeleza kuwa alitegemea serikali imetekeleza hukumu hiyo au kuomba mapitio ya hukumu, badala ya kuilalamikia mahakama.

Anamshauri Prof. Kabudi kuangalia hoja ya msingi ya haki za binadamu, ikiwamo ya mtoto kupata elimu, afya na kumiliki uchumi.

“Serikali ingekata rufani kuomba mapitio ya ile hukumu kama waliona hayakuwa sawa kuliko kulalamika. Inatakiwa kuheshimu maamuzi hayo. Nasikitika kwamba hukumu inayokwenda kulinda na kutetea haki za mabinti zetu inaonekana siyo sahihi,” anasema ole Ngurumwa.

Anasema mabinti wanaoolewa katika umri mdogo ndoa hazidumu na hivyo kuongeza mzunguko wa umaskini kwenye familia.

“Hata kama sheria zimekosewa tunapaswa kuangalia hoja ya msingi ya haki za binadamu kumlinda mtoto, kujenga kielimu na kiafya.

Katika mazingira ya kawaida, binti huyu anakwenda kuolewa ni dhahiri kwamba maisha yake na watoto wake yatakuwa magumu. Kama tuna lengo la kuondoa umasikini Tanzania, lazima tupige vita ndoa za utotoni,” anasema ole Ngurumwa.

Mwanaharakati mtetezi wa haki za wasichana, Rebeca Gyumi, aliyefungua kesi hiyo mara kadhaa anasema ni muhimu iwepo sheria inayomtafsiri mtoto kiuhalisia bila kujali kama yuko shule au nje ya mfumo wa elimu, ili kuzuia ndoa za utotoni.

Rebeca Gyumi (kushoto) na Dk. Ananilea Nkya

“Kuna mkanganyiko ndiyo maana tunatamani sheria ya ndoa irekebishwe kwa sababu mtu akimuoa mtoto chini ya miaka 18 ambaye ni mwanafunzi, anakabiliwa na hatia kwa mujibu wa sheria ya elimu. Lakini akiolewa binti wa miaka 14 aliye nje ya mfumo wa elimu inakuwa ni sawa. Hili ni tatizo,” anasema.

“Inasikitisha mtu aliye chini ya miaka 18 haruhusiwi kuingia mkataba, kupiga kura wala kupewa leseni ya udereva lakini mtoto huyo anaruhusiwa kubeba jukumu la ndoa na familia," anahoji.

Rebecca anasema kifungu cha 13 na 17, kuruhusu binti aolewe akiwa na miaka 14, kinawaumiza zaidi watoto wa maskini wanaokabiliwa na changamato za maisha duni zinazowakwamisha kuendelea na shule.

Watoto wengi wanaoolewa katika umri mdogo wanalazimishwa na si ridhaa yao, kwani baadhi wanaelekezwa kufeli mitihani ili wasiendelee na shule.

Anatoa mfano wa Malawi, Bangladesh, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Zimbabwe zimeidhinisha kuwa umri wa kuoa na kuolewa ni miaka 18, anasema Rebecca.

Anasema baadhi ya nchi hizo zina idadi kubwa ya Waislamu.

Mkuu wa Dawati la Jinsia katika Kanda Maalamu ya Dar es Salaam, Leah Mbunda, anasema matukio mengi ya ukatili wa kijinsia yanatokea kwenye ndoa na kwamba walioolewa katika umri mdogo wananyanyaswa zaidi.

Imefika miaka mitano tangu Mahakama ya Rufani itoe tafsiri ya kisheria kuhusu umri wa mtoto kwamba ni aliye chini ya miaka 18, na kuielekeza serikali irekebishe Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971.