KWAHERI 2024; Uliitikisa, Kariakoo ukikatiza

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:06 AM Dec 25 2024
Maafa ya Kariakoo yaliyoua watu 29.
Picha: Mtandao
Maafa ya Kariakoo yaliyoua watu 29.

SAFARI ndefu ya siku 365 1/4 ya mwaka 2024 iliyojaa milima na mabonde inaelekea ukingoni ili kuukaribisha mwaka mwingine wa 2025 ambao unatarajiwa kuanza Jumatano ya wiki ijayo.

Mwaka 2024 ulikuwa na matukio mengi makubwa yaliyoibua mijadala na hisia mchanganyiko miongoni mwa Watanzania, kuanzia katika siasa na hata vifo vya baadhi ya watu wenye majina makubwa ndani na nje ya nchi.
 
 Baadhi ya matukio katika siasa, yanaanza na Dk. Emmanuel Nchimbi kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Daniel Chongolo aliyejiuzulu mwishoni mwa mwaka 2023. Kwa sasa Chongolo ni mkuu wa mkoa wa Songwe.
 
 Ilikuwa ni Januari 15, 2024 Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM inapokea na kuidhinisha pendekezo la Kamati Kuu ya chama hicho la  kumteua Balozi Nchimbi kuwa Katibu Mkuu wa CCM.
 
 Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao  maalum kilichoketi Zanzibar kikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Samia Suluhu Hassan.
 
 Juni 30, mwenyekiti wa zamani wa Kanda ya Nyasa wa CHADEMA ambaye ni mbunge wa zamani wa Iringa Mjini, Peter Msigwa anatangazwa rasmi kuhamia CCM kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa jijini Dar es Salaam.
 
 Viongozi kujiuzulu na safari hii Julai 29, Makamu Mwenyekiti wa CCM Abdulrahman Kinana, anajiuzulu nafasi hiyo, Julai 29,2024. Ombi lake linaridhiwa na Mwenyekiti wa Taifa, Rais Samia.
 
 Agosti mosi  mwaka unashuhudia wakili Boniface Mwabukusi akichaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), baada ya kupitia misukosuko mingi ikiwamo ya kuenguliwa katika kinyang'anyiro na kukimbilia mahakamani.
 
 Panga pangua ya baraza la mawaziri ilisikika kila wakati. Agosti 14, aliyekuwa Waziri wa Afya Ummy Mwalimu anatumbuliwa, huku nafasi yake ikichukuliwa na Jenista Mhagama ambaye awali alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu).
 
 Novemba 27, uchaguzi wa serikali za mitaa unarindima na CCM inashinda viti vingi, lakini ushindi huo unalalamikiwa kila kona na wadau mbalimbali wa siasa na demokrasia, wakiwamo wanaharakati na viongozi wa dini.
 
 Habari za wasiojulikana kuteka zinazidi kuzagaa, ni Desemba mosi Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo, Abdul Nondo anadai kukamatwa na kuchukuliwa kwa nguvu na watu sita.

Abdul Nondo
Ni tukio la dakika chache baada ya kuwasili katika stendi kuu ya mabasi ya Magufuli Mbezi  Dar es Salaam akitokea Kigoma alipokuwapo kikazi.
 
Desemba 2, Jeshi la Polisi linathibitisha kuwa Nondo amepatikana baada ya kutelekezwa eneo la fukwe za Coco Dar es Salaam akiachwa na watu asiowajua.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa Nondo alimsimamisha bodaboda na kumwelekeza amfikishe katika ofisi za chama chake Magomeni na kufika saa 5:00 usiku na kuonana na viongozi wake kabla ya kupelekwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi wa afya.
 
 Desemba 17, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu anachukua fomu kugombea nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho taifa huku akiwajibu watu wanaokosoa uamuzi wake kuwa jambo hilo si la ajabu na kuwahoji walitaka achukue nani.
 
 Ilipotimia Desemba 21, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, anachukua fomu ili kutetea nafasi yake hiyo inayoishikilia kwa miaka mingi, kitendo ambacho kinaonyesha kutakuwa na ushindani mkali kati ya viongozi hao wawili wenye ushawishi mkubwa ndani na nje ya chama hicho. 

Kitendo cha wababe hao kuchukua fomu ili kuwania nafasi moja, kimeibua makundi mawili ya wanachama na wafuasi wa chama hicho ambao sasa wamegawanyika pande mbili kitendo kinachoashiria kuwa uchaguzi wa mwenyekiti wa CHADEMA taifa utakuwa na ushindani mkali.
      
          MATUKIO YA VIFO

Mwaka umewaachia majonzi wengi, na kubwa ni Novemba 16,  Dar es Salaam na taifa linazizima kwa msiba, kufuatia kuporomoka kwa ghorofa  Kariakoo na kusababisha vifo vya watu 29 waliokuwa wakifanya shughuli mbalimbali za kibiashara.

 Usiku wa kuamkia Novemba 27,  ulijaa simanzi baada ya Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Dunia (WHO) Kanda ya Afrika na Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile, kufariki dunia ghafla  kabla hajaanza kutumikia nafasi mpya ya kimataifa.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali David Musuguri (104), anaaga dunia mwaka huu Oktoba 29,  akipatiwa matibabu katika hospitali jijini Mwanza.

Septemba 6, Mjumbe wa Sekretarieti ya CHADEMA Taifa, Ally Mohamed Kibao, anafariki dunia akidaiwa kutekwa na watu wasiojulikana waliomshusha katika basi la Tashriff akiwa Tegeta  Dar es Salaam, safarini kwenda Tanga, kitendo ambacho kilizua sintofahamu kwa Watanzania, wadau wa siasa na hata leo hakuna aliyekamatwa.
 
 Oktoba 12, Brigedia Meja Jenerali mstaafu Charles Mbuge, aliyewahi kuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na pia mkuu wa mkoa wa Kagera, anafariki dunia, akiwa kwenye matibabu nchini India.
 
 Novemba 9, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru, anaaga dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu nchini India.
 
 Ajali nazo hazikuicha Tanzania salama, Desemba 22, watu 11 waliokuwa wakisafiri kwa basi wilayani Biharamulo mkoani Kagera walifariki.

Heri ya Noeli na pole kwa walioumia moyo mwaka 2004.