HERI YA NOELI, Sikukuu iwe nguzo ya mahaba, upendo kwa wote

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:07 AM Dec 25 2024
Upendo kwa watoto wanaoishi nje ya familia na  mazingira hatarishi ni jambo linalosisitizwa wakati wa sikukuu ya Noeli na Mwaka Mpya.
Picha: Mtandao
Upendo kwa watoto wanaoishi nje ya familia na mazingira hatarishi ni jambo linalosisitizwa wakati wa sikukuu ya Noeli na Mwaka Mpya.

LEO ni Krismas, Jarida la Siasa linawatakia wasomaji wetu, siku kuu njema zenye furaha na amani. Tukitakiana heri hizi kunaambatana na kukumbushana kuwa sherehe hizi zilizoanza usiku wa kuamkia leo hadi tarehe 31, kisha Januari mosi 2025 zisiwe mwanzo wa kufanya maovu.

Baba na mama lakini pia wachumba acheni kuchepuka au kukosa uaminifu. Anza Krismasi, maliza mwaka huu na anza mwaka mpya mkiwa mnathaminiana kila mara.

Mama kubali kuwa maandalizi aliyoyafanya mume wako kwa sikukuu ndio uwezo wake, tumieni mlicho nacho kwa furaha. Kama ni mama watoto au mchumba pia mkubali hali zenu. Kinachotakiwa ni kudumisha  mapenzi na kujali.

Jihadharini msiingie kusaka wapenzi wengine kipindi hiki cha sikukuu kisa kutafuta pesa zaidi.

Wanawake na wanaume wafahamu kuwa nyama ya ulimi ni muhimu wakati wote hata kama mume hana kitu ni muhimu kuongeza upendo na kutiana moyo.

Kwa upande wa wanaume hata kama unaona kuna kasoro kwa mkeo ni muhimu kumpenda. Mpigie simu baba au mama watoto wako au mwenza wako na hata mchumba wakati wote uonyeshe kuwa unajali kwa kujuliana hali iwe mchana asubuhi na hata jioni kabla hajarejea nyumbani.

Katika msimu huu wa sikukuu, maisha ya watu hayawezi kubadilika kwa muda mfupi, hivyo kama hujajaliwa kupata pesa za maandalizi upendo unaweza kuwa silaha ya kuziba udhaifu wenu.

Watoto wakifurahia
Jitahidini kuvumiliana na kukubali kuwa maisha si pesa pekee, mapenzi kwa wanandoa, wachumba pamoja na upendo kwa familia na ndugu bila kusahau amani ya roho na akili timamu vikiongozwa na hofu ya Mungu vinashinda yote.

Wanandoa kama mmekuwa mkikwaruzana  kila wakati, kipindi hiki mnatakiwa kuondoa uhasama kwa kuwa huu ndio wakati mzuri wa kunyoosha mapito na kuwa mwanzo wa kuombana msamaha na kuona raha ya ndoa.

Kumuomba mpenzi wako msamaha sio ishara ya udhaifu, bali kiungo muhimu cha kukoleza penzi lenu kwa baba na mama pamoja na familia yenu.

Kama mhimili wa familia, baba chukua nafasi yako kwa kununua vyakula hata kama ni kabichi ili familia ipate faraja. Ukitaka kupalilia vyema penzi, wanaume ni vizuri mkawasindikiza wake zenu sokoni kununua vitu iwe kuku, kabichi, vitunguu na mchele kutegemea ukwasi wenu.

Haitakua jambo baya kwa wanaume mkiwasindikiza wenza wenu saluni ili wajirembe kwa kusuka nywele  kwa ajili ya sikukuu. Kadhalika baba awahudumie watoto wako wanunulie nguo mpya watoto kama pesa zipo.

Zawadi nzuri hupewa mkeo au mwenza wako, lakini hilo halitakulazimisha kama hauna uwezo.

Baba na mama kumbuka mambo madogo ambayo watu hupuuza ndio hukoleza raha na mapenzi katika msimu huu wa sherehe za sikukuu za Noeli, kumaliza na kuanza mwaka mpya. 

Askofu Waliam Mwamalanga, wa Kanisa la Kipentekoste Tanzania , anakumbusha kuwa maana ya Siku ya Noeli ni upendo wa Mungu kwa mwanadamu na kwamba ni muhimu  mwanadamu anayependwa na Muumba atende upendo huo kwa vitendo.

Katika salamu zake za Krismas, Askofu Mwamalanga, anasema kila mtu amwendee mwenzake hasa wale wanaokaa na chuki na kinyongo kwa muda mrefu asalimiane naye kumaliza chuki iwe ni mke au mume, jirani, watoto na wazazi au walezi.

Anashauri wawapelekee chochote cha thamani na kuwapa hasimu wao ikiwa ni pamoja na kununua kitu kizuri na kuwapatia wale ambao hawawapendi na kufungua ukurasa mpya wa upendo na amani.

Askofu Mwamalanga anakumbusha kuwa kwa wakati huu ambao hali imekuwa ngumu, vilio vya maisha magumu na watu wamefariki kwenye ajali, kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake na kutiama moyo. “Tujali watoto hata kama hatujawazaa na tuhudumie wale ambao hatuwajui.” Anasisitiza.

Kuhusu kujiburudisha anashauri watu wanywe vinywaji laini kama soda, juisi, pia wale matunda na vyakula vyenye lishe kwa sababu pombe kali wamezitumia mwaka mzima. Wawe makini walinde familia zao.

“Familia ziandae chakula siyo kuwaachia watoto wazurure majumbani na kula kwa watu wengine. Waache kusema atakula kwa majirani si kulinda watoto kwanini uwaache kwa majirani?” Anahoji.

Anashauri sherehe za Noeli na mwaka mpya ziwe za mabadiliko kwa watoto zianze kwa walezi na wazazi kwa  kuwavisha mavazi yenye heshima.

 “Wajihisi wafalme wajione wana walezi na wazazi. La muhimu tuwahudumie watoto wasio na msaada mitaani. Na sisi twende kuwatembelea wanaoishi kwenye mazingira magumu na familia maskini popote walipo. Tupeleke upendo.” Anashauri Askofu Mwamalanga.

MPENDE ‘HAUSI GELI’

Ofisa Miradi wa Asasi ya Initiative for Domestic Workers inayotetea watumishi wa nyumbani wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani, Farida Daniel, anakumbusha kuwa kipindi hiki mabosi wawaonyeshe kuwajali wafanyakazi wa ndani na si kuwabagua.

Anawashauri waajiri kuwapa muda wa kupumzika na kufurahia sikukuu za Noeli na mwaka mpya, akiwakumbusha kuwa wapende watoke na watoto wao kufurahia.

“Kuna wengine wanawatumikisha kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa 4:00 usiku ni kazi pekee. Ahudumie wageni, aandae vyakula na mwisho hafurahii Noeli wala mwaka mpya.” Anashauri Farida.

Anawashauri watumishi hao kutimiza wajibu kwa kufanyakazi kwa wakati, kupanga ratiba zao na kufuata maelekezo na si kusikiliza wale wanaowapotosha.