HAPPINESS FREDY: Licha ya kufiwa, hakukata tamaa ni kinara matokeo ya ‘form 4’ 2023

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 06:36 PM Feb 13 2024
Happiness Fredy (18).
PICHA: JULIETH MKIRERI
Happiness Fredy (18).

HAPPINESS Fredy (18), ni mmoja wa wahitimu vinara kwa ufaulu katika mtihani wa kidato cha nne mwaka jana, akibeba alama saba na kupata daraja la kwanza.

Pamoja na yote hayo nawashukuru walimu wa Tumbi kwa jitihada za kufundisha wakati wote wakiwa karibu na wanafunzi ili kuwaandaa na kuwajenga kimasomo," anasema na kuongeza kuwa anatamani kuwa daktari bingwa atakayekuwa karibu zaidi na jamii.

Amemaliza masomo katika Sekondari ya Tumbi iliyoko Kibaha mkoa wa Pwani, mwaka 2023, akiibuka na ufaulu wa daraja la kwanza na kuwa msichana kinara kwenye matokeo hayo.

Happiness amesoma tasnifu au mchepuo wa sayansi, akivuna alama A kwenye Fizikia, Kemia, Bailojia, Hisabati, Kiingereza na Kiswahili, kadhalika akipata B kwenye masomo ya Historia na Jiografia.

Akiishi Mtaa wa Tanita mjini Kibaha anaanza kidato cha kwanza mwaka 2020 akitokea Shule ya Msingi John Bosco ya Kibaha pia.

“Nilianza kidato cha kwanza kwa pigo la kumpoteza baba yangu mzazi Fredy Godfrey, haikuwa rahisi kukubaliana na hali hiyo na hapo ndipo historia ya maisha magumu ilipoanza kutokana na misuguano ya kifamilia,” anasema.

Anaongeza kuwa baba yake mjasiriamali wa kuuza vinywaji mbalimbali alikuwa nguzo ya familia na mhusika mkuu wa elimu yake na alipofariki maisha yakabadilika.

Anasema mama yake hakuwa mwajiriwa wala mjasiriamali na kwa ujumla alimtegemea mume wake pekee na alipofariki ilikuwa pia ni mtikisiko.

“Kutokana na maisha nyumbani kuwa magumu nikwenda shuleni kwa msaada wa majirani ambao walikuwa wakinunulia sare za shule, kunilipia nauli na mahitaji ya shule.” Anaongeza. 

"Mama hakuwa na biashara wala ajira baada ya baba kufariki alianza kutumia cherehani kushona nguo akiweka viraka ambavyo vilimpa vijisenti kidogo vilivyotusaidia kupata chakula tu," anasema Happiness. 

Anaeleza kuwa familia yao iliishi muda mrefu katika mazingira magumu kutokana na kukosa msaada wa wanafamilia waliokuwa wanataka kuwapora mali za baba yao ikiwamo nyumba.

 “Uvumilivu ulifika ukingoni baada ya kufika kidato cha tatu mambo yakazidi kuwa magumu nikatoroka nyumbani kwenda kuishi jirani na shuleni, tena karibu ambako nilikuwa nakwenda na kurudi kila siku.” 

"Nilitoroka nyumbani baada ya kuona mateso na vurugu za familia zikiendelea nikaenda kuishi sehemu ambayo hakuna aliyenijua. Nikiwa huko  nilikwenda kila siku shuleni mpaka nimemaliza kidato cha nne," anasema Happness, lakini akakataa kuzungumzia eneo hilo.

 Mahali alipokuwa anaishi Happiness napo licha ya kwenda shuleni, anasema palimpa wakati mgumu ni gharama za usafiri. Kila siku alilazimika kupanda magari manne na bodaboda kwenda shule na kurudi nyumbani.

 

SHIDA BARABARANI

 

Amekumbana na vikwazo vingi ikiwamo kunusurika ajali na ushawishi wa wanaume ambavyo vingekatiza masomo yake.

Pamoja na mambo kuwa magumu aliweka malengo ya kutoka nyumbani saa 11 alfajiri kuelekea shuleni na kurudi saa 3:00 usiku, akiazimia kuwahi na bila kukosa kipindi darasani.

Anasema akiwa shuleni mara nyingi alisahau magumu anayopitia, akiwahi kuingia darasani mpaka saa 8:30 na kusoma hadi jioni lakini pia kufanya majadiliano ya masomo na mwenzake.

 “Majadiliano yamenijenga, kunipa ushupavu, kujiamini na kuniimarisha katika masomo huku nikiweka lengo la kufaulu ili niendelee na masomo ya juu.”

 Anasema matokeo yalipotangazwa yalimpa faraja, furaha na matumaini tena kumsahaulisha magumu aliyokumbana nayo wakati akisoma.

 Anaibuka na alama A nane na B mbili na hivyo kumpa nafasi katika Shule ya Tumbi Sekondari kuwa msichana kinara kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha kwanza.

 Binti huyu wa kwanza kwenye familia yake ya watoto watatu anaishukuru serikali kwa kujenga shule za kata na kuendelea kugharamia masomo, akieleza kuwa pengine bila kuwapo kwa shule hizo asingesoma.

“Kilichonipa ushindi katika safari hii ni kukubali kuwa serikali inatusaidia, lazima kusoma. Nitumie muda kujifunza, kushauriana na kushirikiana na walimu na wenzangu na kuwa na msukumo wa kutaka kufaulu.”

 Pia, anasema aliweka malengo ya kupata daraja la kwanza japo hakuwahi kuwashirikisha wengine lakini pia amekuwa akimtanguliza Mungu katika kila jambo kwani pamoja na misukosuko ya maisha aliyopitia Mungu amemvusha.

"Pamoja na yote hayo nawashukuru walimu wa Tumbi kwa jitihada za kufundisha wakati wote wakiwa karibu na wanafunzi ili kuwaandaa na kuwajenga kimasomo," anasema na kuongeza kuwa anatamani kuwa daktari bingwa atakayekuwa karibu zaidi na jamii.

 WASICHANA VINARA

Mkuu wa Sekondari Tumbi Fidelis Haule, anasema wasichana waliofanya mitihani ya kumaliza kidato cha nne mwaka 2023 walikuwa 34.

Kati ya hao waliopata ufaulu wa daraja la kwanza ni 14, daraja la pili ni 16 wakati daraja la tatu ni watatu na daraja la nne yuko mmoja akiwasifu kuwa ufaulu wao ni wa juu sawa na  asilimia 99.

 Haule anasema siri ya ufaulu kwa wasichana hao ni juhudi darasani, nidhamu, kusikiliza walimu pamoja na motisha mbalimbali zinazotolewa na serikali kwa walimu ikiwapo kuwashika mkono na kuwaongezea hamasa ya kazi.

 Haule anaongeza: “Namshukuru Makamu wa Rais, Dk.Philip Mpango, Februari 4,2023 alipita shuleni hapo na kutoa motisha ya Shilingi milioni 50 kwa walimu baada ya kuridhishwa na matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2022.”

 Anasema motisha ya Makamu wa Rais imekuwa chachu ya kuongeza morali kwa walimu katika ufundishaji na kwamba zawadi pekee ilikuwa kuongeza ufaulu.

 Haule anasema Tumbi ina vifaa vya kutosha vya kufundishia, walimu pamoja na miundombinu bora iliyokarabatiwa na serikali hivi karibuni.

 "Ufaulu huu ni jitihada za serikali maana imefanya kila kitu, kukarabati miundombinu ya shule yetu tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ya kuboresha elimu," anasema Haule.

 Diwani wa Kata ya Tumbi (CCM), Raymond Chokala, anasema ufaulu wa wasichana Shule ya Tumbi umetokana na ushirikiano baina ya walimu, wazazi na wanafunzi.

 Chokala, anaomba ushirikiano huo uendelee ili shule kinara katika matokeo ya miaka ijayo huku akimpongeza Mkuu wa Shule Haule kusaidia wanafunzi, kushirikiana na walimu kuboresha elimu.