Dozi moja inavyotosha kufanikisha kuzuia saratani shingo ya kizazi

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 12:40 PM Apr 25 2024
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Mwanza, wakiwa katika maadhimisho ya chanjo ya HPV, katika viwanja vya Furahisha.
Picha: Yasmine Protace
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Mwanza, wakiwa katika maadhimisho ya chanjo ya HPV, katika viwanja vya Furahisha.

NI maadhimisho ya ‘dozi ya chanjo ya HPV’, inayomkinga mtoto wa kike asipate ugonjwa wa saratani ya mlango wa shingo ya uzazi.

Chanjo hiyo ya HPV inawalenga watoto wenye umri kati ya miaka tisa na 14, ambayo Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, anasema kuwa dozi moja inatosha kumkinga msichana kupata ugonjwa wa Saratani ya Mlango wa Kizazi. 

Waziri Ummy anayaongea hayo kwenye uzinduzi wa Maadhimisho ya Dozi moja ya chanjo ya HPV kwa wasichana, akinena ni jukumu la wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto kupata chanjo hiyo. 

Ni hafla iliyofanyika katika Viwanja vya Furahisha Wilayani Ilemela, Mwanza akiwa na ufafanuzi: “Wataalamu wetu ambao wanatoka kwenye Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR). 

“Wametuhakikishia kuwa dozi moja ya chanjo ya HPV inatosha kumkinga msichana kupata saratani ya mlango wa kizazi.” 

Anasema awali dozi zilitolewa mbili, ya pili ikiwa ni miezi sita akipelekewa binti, hata hivyo wengi hawakurudi kumalizia. 

Lakini anaeleza mbadala uliopo ni kwamba, hivi sasa anasema wanatoa dozi moja, inayotosha kuwakinga wasichana dhidi ya maambukizi ya saratani ya mlango wa kizazi.  

Waziri anaeleza saratani inayoongoza kuwatesa Watanzania ni ‘Mlango wa Kizazi’ anayosema katika kila wagonjwa100, wako 23 wagonjwa wa Saratani ya Mlango wa Kizazi.  

Anaorodhesha saratani zinazofuatia kwa ukubwa ni inayohusu: Mfumo wa Chakula, asilimia 11; matiti asilimia 10.4; tezi dume asilimia 8.9. 

Pia, Waziri anatoa wito kwa wazazi na walezi nchini, kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo zote wanazopaswa, ili wanufaike na kinga dhidi ya maradhi yaliyotajwa, ikiwamo lengo kubwa la kuwakinga na magonjwa, yakiwamo haya ya saratani pamoja na kuwakinga na vifo vinavyoweza kuzuilika na chanjo.  

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa Mwanza, Saidi Mtanda atahakikisha watoto wote wenye umri wa kuanzia miaka tisa hadi 14, wanapata chanjo hiyo ili kufikia malengo.  

“Kwa mwaka 2022/23 Mkoa wa Mwanza ulifanikiwa kuchanja watoto zaidi ya laki Mbili sawa na asilimia 107 kati ya walengwa waliotarajiwa kuchanjwa ni laki 191,440 wenye umri chini ya mwaka mmoja, tumefikia malengo na kuyavuka,” anasema. 

Mkazi wa Jiji la Mwanza Amina Said, anasema kutolewa kwa chanjo hiyo ni moja ya mapambano ya kumkinga mtoto wa kike asipate saratani ya mlango wa kizazi. 

Anasema elimu juu ya chanjo hiyo inatakiwa kutolewa mara kwa mara ili jamii iendelee kuelewa umuhimu wa chanjo hiyo. 

"Mimi nina mtoto wa kike ana umri wa miaka name,lakini sina  elimu yoyote, kuwa anapofikisha miaka tisa anatakiwa kupatiwa chanjo hiyo," anasema. 

Anaongeza kuwa, serikali inapambana kuwahakikishia wananchi wake wawe na afya njema, hivyo ana rai elimu iendelee kutolewa kwa jamii, ijue umuhimu wa chanjo. 

Aziza Jumanne, mkazi wa Mwanza anaitaja chanjo hiyo kuwa mkombozi kwa wasichana wenye sifa ya kupata chanjo hiyo, akiishauri jamii izingatie jinsi ya kuwasaidia watoto wa kike wasipate ugonjwa huo. 

"Kila mzazi ambaye ana mtoto wa kike aliye na sifa za kupata chanjo, awapeleke kupata chanjo hiyo," anasema, kuwa watoto wanapopatiwa chanjo, wananudhurika kwa maradhi hayo.

 Anthony Andrew, mkazi wa Maduka Tisa, jijini Mwanza anasema ni wakati wa wazazi na walezi kuachana na mila potofu dhidi ya kuwapo chanjo hizo na kinachotakiwa ni kuisaidia serikali, ili watoto wapate waelewe.

 Andrew anakumbusha chanjo inatolewa bure na inabaki  jukumu la walezi na wazazi kujitokeza na watoto wao waweze kupatiwa chanjo hiyo. 

"Tumekuwa tunasikia kutoka kwa wataalamu wetu wa afya, magonjwa sugu yanayo changia vifo kwa jamii. Katika magonjwa hayo, saratani nayo ipo," anasema, akiwa na ufafanuzi.

 Anaongeza kuwa, saratani zote zina changamoto zake, kama mtu atachelewa kupata matibabu kwa wakati anayonafasi kubwa ya kupoteza maisha.