DIWANI KULISHWA MATOPE, Viongozi wajihoji

By Dk. Felician Kilahama , Nipashe
Published at 11:06 AM Dec 25 2024
Ni msoto kwa wakazi wa Msumi na Madale Dar es Salaam, kusafiri kutokana na kukosa daraja kwa mwaka sasa.
Picha: Mtandao
Ni msoto kwa wakazi wa Msumi na Madale Dar es Salaam, kusafiri kutokana na kukosa daraja kwa mwaka sasa.

WIKI iliyopita Desemba 18, zinasikika taarifa kuwa wananchi wamemburuza diwani wao kwenye matope na sababu ya kufanya hivyo zikatajwa kuwa ni kutoridhishwa na utendaji wake, hali mbaya ya barabara katika eneo lao na kwa kifupi kutokuwajibika.

Ukweli ni kwamba hata sehemu wanazoishi watu wengine wengi  hali za barabara hasa nyakati za mvua ni ‘kichefuchefu’ pamoja na kero nyingi mitaani. Kuna wanaotupa taka bila kujali usafi wa mazingira na kutiririsha majitaka ovyo nyakati za mvua ikiwamo kufungua makaro ya taka za vyooni.

Kadhalika, akasikika ‘kiongozi kigogo’ akitoa pongezi tena, akisifia kitendo kilichofanywa na wananchi wa eneo hilo kwa diwani wao nikabaki nimeduwaa kidogo nikijiuliza  kufanya hivyo ni sahihi?

 Hata hivyo, kiongozi huyo shupavu akaongeza kusema ‘viongozi wengi hawawajibiki ipasavyo’ nami nakubaliana na hoja hiyo. 

Hali ya viongozi kutowajibika kikamilifu, inapelekea wananchi kushikwa na hasira na kufanya maamuzi magumu kama hilo la kuburuzana kwenye mapote. Kadhalika, akaongeza kuwa mwaka wa fedha 2023/2024 kiasi cha shillingi bilioni 20  zilirudishwa hazina,  kisa hazikutumika wakati zilitakiwa zitumiwe kuwaletea maendeleo au kuimarisha huduma za kijamii katika halmashauri husika. 

Baada ya tafakuri fupi ndipo nikawaza je, tatizo au changamoto Tanzania ni upatikanaji wa fedha au ni ukosefu wa uongozi imara? Kufikiri  ni kitu kimoja na matokeo yake ni kitu kingine. Hata hivyo, sikuwa na jibu kamili.

Kwanza, utwala, uongozi wa nchi  umejengeka kwenye misingi ya sheria na katiba ya  Tanzania ikiwa ndiyo sheria kuu ikifuatiwa na sheria, kanuni na taratibu za kisekta, kisiasa na kitaaluma. Vilevile, kuna viongozi wa kisiasa na wa  kiutendaji lakini pia wapo wataalamu kutokana na taaluma mbalimbali zikiwamo za kijamii, kisiasa, kisayansi, kisaikolojia, kidini na mifumo ya kijadi pia.

Taifa  hili  ni tajiri na siyo maskini hivyo fedha na rasilimali nyingine kuanzia watu, ardhi na mazao vyote ni fedha toshelezi, changamoto zilizopo zinatokana na binadamu wenyewe. Mathalani, kama halmashauri ikipokea fedha ilizoomba kuwaletea maendeleo na kuimarisha huduma za kijamii katika eneo lake kulingana na mipango iliyopeleka serikali kutoa hizo fedha; halafu zisitumike hadi kurudishwa, ni jambo la kutatanisha. 

Je, kulikuwa na makosa katika kupanga maana ni pamoja na kuchagua nini cha kufanya, nini kisifanyike, iweje zisitumike ilivyotarajiwa? Wananchi wanaposikia fedha nyingi kiasi hicho hazikutumika wakati uhalisia wa mambo katika maeneo mbalimbali kwenye sehemu zao ni ‘kero’ tupu zisizopata ufumbuzi wa haraka, inasababisha  ‘sintofahamu’ hadi kufanya maamuzi yasiyofaa ambayo pia ni kinyume na utawala wa kisheria.

Viongozi wa sekta na wizara mbalimbali, mashirika, mikoa na halmashauri Tanzania Bara, nimekuwa nikiwasikia wakisema “… namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, Mama yetu mpendwa amekuwa akitoa fedha nyingi kuwaletea maendeleo Watanzania...” 

Hili kisiasa ni sawa, lakini kiutendaji pamoja kwamba Rais ni Mtendaji (Executive President) lakini mifumo ya kiutawala na kiutendaji ipo hivyo, inatakiwa ifanye kazi ipasavyo. Mathalani, bunge la bajeti likipitisha makadirio na matumizi ya fedha kwa mwaka husika hutayarishwa muswada wa fedha ambao ukiridhiwa na wabunge na hatimaye kuwekwa saini na Rais, inakuwa ndiyo sheria ya fedha kuhalalisha matumizi ya kiasi kilichopitishwa na bunge kwa mwaka huo.

Baada ya hapo, wizara, mashirika, mikoa, halmashauri  pamoja na bunge na mahakama huanza kutekeleza shughuli zilizoanishwa kwa kutumia fedha zilizoidhinishwa. Kupitia Sheria ya Fedha kwa kupindi husika. 

Hata hivyo, katika kuwahangaikia wananchi wa maeneo tofauti Rais, anaweza akapata fedha au misaada kutoka nchi marafiki au hapa nyumbani  ambazo ni nje ya bajeti  na kwa matashi yake akazitoa zitumike kwa faida ya wananchi wa eneo fulani.

 Ikitokea ikawa hivyo, hata mimi nisingesita kumshukuru kwa jitihada kama hizo zenye dhamira njema kwa Watanzania.

Viongozi wa kisiasa kama madiwani na wabunge kupitia maeneo yao wanawajibika kukusanya kero na kuzifanyia kazi na kukazana fedha zitapatikane kupitia bajeti za serikali, ili kuondoa kero za wananchi kwa kutumia fedha zilizoidhinishwa rasmi au zilizopatikana kihalali kupitia mifumo tofauti.

 Iwapo hatua hazichukuliwi haraka na kero kukithiri sehemu kadhaa nchini motokeo ni mfano wa barabara mbovu kupelekea wananchi kumwadhibu diwani kinyume na sheria na taratibu. Kimsingi, wanaorudisha fedha bila kuzitumia ilivyotarajiwa siyo wanasiasa bali viongozi watendaji iwe wizarani au kwenye halamashauri husika. 

Ukifuatilia jambo lilo utagundua ni watumishi na watendaji wa umma wenye mizozo binafsi itokanayo na migongano ya kimaslahi kiasi cha kuwaadhibu wananchi kwa kutotumia fedha zilizoidhinishwa zitumike kuwaondolea kero sehemu husika.

Miaka ya karibuni ‘pepo’ la ubinafsi na kutowajibika ipasavyo kwa baadhi ya viongozi wa umma limekuwa changamoto kubwa kwenye usimamizi wa rasilimali fedha katika sekta ya umma. Fedha zikitolewa na hazina au kama inavyosemwa na Rais, zitumike kulingana na kusudio lenyewe mfano, kujenga au kuimarisha miundombinu ya barabara, kilimo, umwagiliaji, kusambaza maji au umeme, afya na elimu kwa jamii mijini na vijijini.

 Kusiwepo na ‘roho’ kwa baadhi ya viongozi kutaka kujinufaisha wanapohoji nafsini mwa fedha zikitumika binafsi nitapata nini na au nitafaidika vipi? Hizo ni ‘roho’ zilizojaa ‘uovu’ zinazofurahia au kushabikia ‘kero na mateso’ kwa wananchi wakati wenyewe watendaji na watumishi wanatakiwa kuwajibika kuwatumikia wananchi ipasavyo. 

Nionavyo mimi suala la kurejesha bakaa ya fedha kila mwisho wa mwaka wa fedha wa serikali ni la kiutendaji si la kisiasa. Lakini inapotokea fedha zikarejeshwa kuwepo sababu za msingi zisizoepukika kiutendaji au kiutawala. 

Inapotokea kushindwa kutumia fedha zilizoidhinishwa na bunge zisitumike kwa sababu baadhi ya viongozi na watendaji wanakwamisha na kupelekea suala hilo kutokea kinyume na matarajio ya wananchi  kwa kujali maslahi binafsi kuliko  ya umma na taifa kwa ujumla, huo ni ‘ufisadi’ mkubwa  hatua kali zichukuliwe. 

Kadhalika,  vyombo vya habari na mitandao ya kijamii  vinasema mgonjwa analetwa kwenye zahanati, kituo cha afya au hospitali akiwa mahututi, lakini wataalam husika wanakataa kumtibu wakidai malipo kwanza na kusababisha kifo. Watanzania utu na kuthaminiana pia  kuhurumiana na kupendana kama binadamu vimepotelea wapi au ndiyo matokeo hasi ya utandawazi, kupenda fedha sana kuliko ubinadamu? 

Kimsingi viongozi, watumishi wanaoteuliwa kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma kwenye wizara, mashirika, mikoa, wilaya na halmashauri wawe watumishi wenye mioyo iliyobeba maslahi  ya umma na taifa kuliko maslahi binafsi.

 Kiongozi wa aina hiyo hatafurahia kurudisha fedha hazina wakati eneo analolisimamia limesheheni kero lukuki hivyo atafanya kila linalowezekana fedha zitumike kihalali na kwa faida ya wengi. 

Viongozi ‘kutunishiana misuli’ haina tija kwa jamii pia wananchi na viongozi kuburuzana kwenye matope au kukejeliana siyo jambo jema. Isipokuwa wote kwa pamoja tunatakiwa tushirikiane na kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kila Mtanzania anaishi kwa amani na kupata mahitaji ya msingi mfano, chakula, mavazi, mahali pa kuishi, afya njema, kufanyakazi kwa bidii.

Watoto wakipata elimu stahiki na miundombinu kujengwa ipasavyo kote nchini. Fedha ziwe na matokeo chanya ya jasho letu na kila mtu akijivunia kipato halali pamoja na kuwa na hofu ya Mungu.