Disco la zamani, spika moja juu mtini, nyingine kwenye mtungi

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:23 AM Jan 25 2025
Disco la zamani, spika moja juu  mtini, nyingine kwenye mtungi.
Picha: AI
Disco la zamani, spika moja juu mtini, nyingine kwenye mtungi.

MAISHA yanakwenda kasi sana. Hivi sasa disco linatumia vyombo vingi vya kisasa, muziki ukipigwa unaweza kusema kuwa labda kuna dansi linapigwa laivu.

Kwa sasa kuna vyombo ambavyo vinafanya muziki uwe na sauti kubwa zaidi na nzito, kiasi kwamba unaweza hata kukuzibua masikio.

Disco la sasa liwe kwenye kumbi za starehe, harusi, ubatizo, kipaimara ya sherehe zingine za kijamii, linaweza kupigwa sehemu lakini watu waliokuwa kilometa nyingi mbali wakasikia.

Ni kwa sababu ya teknolojia kuzidi kukua. Kila kukicha wataalamu wanatengeneza vyombo ambavyo vitaufanya muziki uvutie zaidi. Ndiyo maana zamani muziki ulikuwa uko kwenye mfumo wa mono, lakini baadaye wataalamu wakatengeneza vifaa ambavyo muziki ukawa unasikika kwenye mfumo wa stereo.

Mono ni mfumo wa sauti ambayo inasikika bila kuchujwa. Kama ni muziki unasikika jinsi ulivyo bila sikio kuchambua kama kuna vyombo gani vinapigwa, au sauti.

Mfumo wa stereo inaonyesha sauti iliyochujwa. Wanamuziki wenyewe wana msemo wao kuwa 'imeondolewa mafua' Sauti ya mono wanaiita yenye mafua. Hata muziki ukisikika kwa mfumo wa stereo msikilizaji atasikia sauti nyororo, na vyombo vilivyotumika vikijipambanua na kusikika vizuri kabisa.

Wataalamu siku zote hawalali. Wakaendelea kuumiza kichwa ndipo walipogundua kuongeza vifaa vya kuongeza sauti kama vile 'booster Amplifier', 'subwoofer amplifier', na vingine vingi vinavyofanana na hivyo.

Hata redio za kisasa maarufu kama 'sabufa' zina sauti kubwa, nzuri, zilizochujwa na mpangilio mzuri wa besi, kiasi cha kuweza hata kuchezesha disco.

Zamani haikuwa hivyo. Ni kweli vyombo vya muziki vilikuwa na sauti, lakini hazikuwa na mfumo mzuri kwenye mpangilio au mfumo wa besi.

Sasa hebu tuhame na kurudi miaka mingi nyuma ambapo watu walipokuwa wakitaka kufanya sherehe za kijamii, iwe za kumaliza shule, chuo, harusi, au disco tu la kawaida.

Achana na zile disco za kwenye kumbi. Nalozungumzia mimi ni lile la mitaani na vijijini.

Mashine moja ya muziki maarufu wakati huo kikiitwa 'record Player', ndiyo iliyokuwa inatumika.

Ni kitu mfano wa sanduku ambacho kilikuwa kinazungusha santuri iliyorekodiwa na bendi mbalimbali za muziki. Sanduku hilo lilikuwa likifunikwa na spika zake mbili.

Zile spika zilikuwa na sauti, lakini zilikuwa na stereo sana, lakini hazikuwa na besi.

Kama muziki unasikilizia nyumbani wala haikuwa na tatizo. Lakini kama ni sherehe na hakukuwa na chombo kingine cha kuweza kupiga disco, basi 'player' ilifanyiwa utaratibu itoe sauti kubwa zaidi ya ila ya kawaida.

Hapo ndipo utatafutwa mtungi mkubwa, na kile kisanduku cha spika ya kwanza ikawekwa ama juu ya mtungi au ndani, itategemea na mtaalamu mwenyewe atakavyoweza kuiseti.

Lengo hapo ni kupata mdundo wa besi ili kunogesha au kupata ladha halisi ya wimbo, pamoja na kuweza kuchezeka kwa raha.
Muziki bila besi ni kama chakula bila chumvi, ndimu, pilipili au kachumbari. Na kweli spika ikiingizwa kwenye mtungi na muziki ukianza kupigwa sauti ya besi inasikika kutokana na sauti ya muziki kuzongwa mtungini.

Kuna 'player' zenye spika moja, lakini pia zipo ambazo zina spika mbili. Sasa hizi moja itawekwa kwenye mtungi na nyingine juu ya mti.
Ile inayowekwa juu ya mti lengo lake ni kwamba wote waliokuwa hapo wausikie muziki. Ikikaa chini na kwa vile kuna mkusanyiko wa watu, basi watu wa pande zikingine hawatausikia vizuri. 

Spika inapandishwa juu ya mti, inafungwa, disco linaanza. Sababu nyingine watu wa mbali kidogo nao waonje ladha ya muziki wa kwenye disco hilo.

Hayo ndiyo yalikuwa na mahesabu, ufundi na ujanja wa vijana wa miaka ya 1960, 1970, 1980, hadi 1990 mwanzoni.

Hili sasa ndiyo lilikuwa linaitwa 'disco vumbi'. Maana watu kutoka sehemu mbalimbali au vijiji mbalimbali walimiminika kujuika kwenye sherehe hizo. Wanapotoka hapo ni vumbi tu mtindo mmoja, miguuni, kichwani hadi kwenye kope.  

Ilipofika katikati ya miaka ya 1990, redio kaseti kubwa, zenye maspika makubwa zilianza kuingia nchini na kuchukua nafasi ya 'player'. Zenyewe sasa zilikuwa na sauti kubwa zaidi. Ziliboreshwa na kuwa na besi, pamoja na vifaa vya kuchuja sauti na kutaka kuifanya vyovyote unavyotaka.

Hapa ndipo yalipokuja mageuzi ya kutoka kwenye 'record player' hadi kwenye redio kaseti.

Na hata mauzo ya santuli yalianza kupungua, kwani watu walinunua kanda za kaseti badala yake.
Kila mwenye pesa sasa alitaka kumiliki redio kaseti badala ya 'player'. 

Hata hizo redio kaseti zenyewe muda wake ulipokwisha watu waliziweka pembeni na kifaa kinachoitwa 'music system' kilianza kuchukua nafasi yake. Mpaka sasa redio za aina hiyo zipo. Ila 'subwoofer', maarufu kama 'sabufa' nazo kwa sasa zipo kwenye chati.

Kwenye disco mitaani kwa sasa zinasimamishwa spika kubwa na Ma-DJ wa kisasa wana mashine maalum za kupigia disco, na wengine wana kompyuta mpakato maarufu kama 'laptop' ambazo wanakuwa wamezihifadhi nyimbo zao. Disco likipigwa hadi mtaa wa 12 wanasikia.

Tuma meseji 0716 350534