CHADEMA na polisi kutunishiana misuli

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:41 AM Sep 25 2024
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe akiwa chini ya ulinzi wa polisi, alipokamatwa eneo la Magomeni, Dar es Salaam jana. Eneo la Magomeni ndiko kunadaiwa maandamano hayo yangeanzia.
PICHA: MIRAJI MSALA
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe akiwa chini ya ulinzi wa polisi, alipokamatwa eneo la Magomeni, Dar es Salaam jana. Eneo la Magomeni ndiko kunadaiwa maandamano hayo yangeanzia.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Jeshi la Polisi wameanza wiki kwa kutunishiana misuli baada ya serikali kupiga marufuku maandamano ya chama hicho, lakini viongozi wake wakaendelea kuhamasisha wanachama waandamane.

 Vuta ni kuvute hiyo, inasababisha viongozi wa juu wa chama hicho kukamatwa, akiwamo Mwenyekiti Taifa Freeman Mbowe na Makamu Tundu Lissu, lakini baadaye wakaachiwa.
 
 Tukio hilo linalotokea jijini Dar es Salaam juzi, na baadhi ya wachambuzi wa siasa wanalizungumzia sakata hilo wakisema katiba inaruhusu lakini mazingira hayakuwa rafiki.

  “Maandamano ya amani ni haki ya kikatiba ya kuelezea hisia zao, lakini hali ingekuwa tofauti kulingana na mazingira yaliyopo sasa,” anasema Mwenyekiti wa Taasisi ya Utawala Bora na Maendeleo Tanzania (CEGODETA), Thomas Ngawaiya.

Anafafanua kuwa hatua zinazochukuliwa na polisi kuzuia maandamano hayo ni muhimu kwa wakati huu.
 
 Ngawaiya ambaye ni kada wa CCM, lakini mbunge wa zamani wa Jimbo la Moshi Vijijini 2000-2005 NCCR-Mageuzi, anasema viongozi wa CHADEMA walishinikiza maandamano kwa sababu ya kifo cha hivi karibuni cha mwanachama wao, Ali Mohamed Kibao.

Kibao, mjumbe wa halmashauri kuu ya CHADEMA, alitekwa na kuuawa kisha mwili wake kupatikana  Ununio nje kidogo ya Dar es Salaam. Alichukuliwa kwa nguvu kutoka kwenye  basi na watu wenye silaha, waliosaidiwa na mwingine aliyejifanya abiria.

Mwili wake ulimwagiwa tindikali usoni kwa mujibu wa uchunguzi wa awali wa mwili wake.

 "Maandamano ya amani ni haki kikatiba, lakini naamini hali ingekuwa tofauti kulingana na mazingira yaliyopo. Hivyo, polisi walikuwa na ulazima wa kuyazuia," anasema Ngawaiya.
 
 Anafafanua kuwa, kwa matukio ya kutekwa au kuuawa kwa baadhi ya wanasiasa huku tuhuma zikielekezwa kwa polisi, kunaweza kuibua hasira na kusababisha watu kuumia na hata kushambuliwa.
 
 "Kwa mfano, mtu anaweza kuua bila kukusudia, kwa kawaida polisi wanamweka ndani kwa ajili ya usalama wake, kwa sababu akiachwa mitaani, raia wanaweza kumuumiza," anasema.
 
 Ngawaiya anasema, mazingira kama hayo ni sawa na tukio la maandamano ya CHADEMA yaliyopigwa marufuku, akisema  iwapo wangeruhusiwa pengine wangeibua hasira kali kwa watu ambao huenda wameathiriwa kwa kupotea ndugu zao na kusababisha vurugu.
 
 Kada huyo anasema, jambo la msingi ni kusubiri vyombo vya dola vimalize uchunguzi ili kuepusha mvutano usio wa lazima kati ya chama na taasisi hizo.

 "Ni muhimu wanasiasa kuzingatia wakati sahihi wa kuandamana. Mbona wameandamana maeneo mbalimbali ya nchi huku wakilindwa na polisi, kwanini wanapozuiliwa wasiheshimu? Polisi hawawezi kuwazuia bila sababu. Wameona kuna viashiria hatarishi," anasema.
 
  NI HAKI LAKINI
 
 Mchambuzi wa siasa Said Msonga, anasema pamoja na kwamba ni haki kikatiba kuandamana, pengine haukuwa wakati sahihi kwa chama hicho kuitisha maandamano.
 
 Anasema, mvutano kati viongozi wa CHADEMA na polisi, ulitosha kwa chama hicho kutulia kwanza badala ya kulazimisha kuandamana wakati kukiwa na sintofahamu.
 
 "Sijui maandamano yao yalilenga nini. Kama ni mauaji, serikali imeanza kuchukua hatua za uchunguzi, ingekuwa ni busara kusubiri kwanza," anasema Msonga.
 
 Mchambuzi huyo anafafanua kuwa wana CHADEMA wangesubiri matokeo ya uchunguzi, na kuongeza kuwa wasiporidhika waitishe maandamano.
 
 "Ingawa kuandamana ni haki ya kikatiba, sidhani kwamba ni sahihi kufanya hivyo, wakati uchunguzi ukiendelea, kwani ni sawa na kuzidisha mvutano usio wa lazima," anasema.
 
 Msonga anasema, mivutano haileti muafaka, badala yake panapokuwapo sintofahamu, ni muhimu kukutana na kujadiliana ili kufikia mwafaka, kwa maslahi ya taifa.
 
 "Maandamano yapo kikatiba, lakini yasilazimishwe pale linapojitokeza jambo ambalo halijawa sawa, badala yake limalizwe kwanza," anasisitiza.
                    
  FALSAFA R4 KWANZA

 Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Magdalena Sakaya, anasema, falsafa ya R4 ya Rais Samia Suluhu Hassan  ni vyema iheshimiwe.

 "Kwa tukio la CHADEMA na polisi, sioni uvumilivu wala  maridhiano hapa. Kwa ujumla sijaona falsafa ya Chama cha Wananchiikitekelezwa …," anasema Magdalena.
 
 Anaongeza kuwa anatamani kuona R4 za Rais zikitekelezwa kwa vitendo badala ya polisi kutumia nguvu kubwa kuzuia maandamano, wakati jukumu lao ni kuyalinda ili wananchi wafikishe hisia zao kwa viongozi.
 
 "Imenisikitisha kuona jinsi polisi walivyotumia nguvu kubwa kumdhibiti Mbowe wakiwa na bunduki kwa mtu asiye na hata kijiko mkononi bila kujali kwamba ni kiongozi mkubwa ana heshima yake," anasema.
 
 Anasema, viongozi wa serikali wamsaidie Rais Samia kutimiza R4 kwa ustawi wa taifa, kwa kuzingatia kuwa Tanzania ni nchi ya wote wakiwamo wanasiasa, wasio wanasiasa, wenye dini na wasioamini.

 "Hakuna anayependa vurugu, kwa kuwa miezi ya hivi karibuni polisi walilinda maandamano ya CHADEMA, waendelee kufanya hivyo, badala ya kutumia nguvu kubwa kudhalilisha upinzani," anasema.
 
 Mwanasiasa huyo anasema si sahihi polisi kutumia nguvu kubwa kwa jambo la kawaida na kufafanua kuwa wangemwita Mbowe kistaarabu ili kumtunzia heshima badala ya kumzingira wakiwa na bunduki.
 
 "Inashangaza kuona Mtanzania ambaye hana silaha kuzingirwa kama mhalifu. Hebu tuheshimu falsafa ya Rais, iwe dira ya kuturudisha kwenye mstari," anasema Magdalena.