KASHINDE Mwendesha (20) ni shujaa aliyeruka na kuchomoka viunzi akiyakimbilia mafanikio ya elimu na sasa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), akisoma shahada ya maendeleo ya jamii.
Ameishi uhamishoni kwa miaka miwili akijiokoa na balaa la kuozwa na miaka 17 alipomaliza kidato cha nne. Ni ndoa zinazoathiri mabinti vijijini wanaolazimishwa kuolewa licha ya kuwa wadogo kwa kisingizo cha kupata mali au kuenzi mila potofu.
KILICHOMKUTA KASHINJE
Akizaliwa katika Kijiji cha Nyikoboko wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga, Kashinje anapotimiza miaka 17, anafaulu mtihani wa kidato cha nne kwa kupata daraja la pili, lakini familia yake haikuona umuhimu wa kuendelea na kidato cha sita, ikishawishika na mahari ya Sh. 200,000 na ng’ombe saba.
Kashinje anasema, awali aliweka msimamo pamoja na mama mzazi kuwa lazima atimize malengo ya kielimu afike chuo kikuu, ndipo aolewe. Mama alimuunga mkono na kumsisitiza kuongeza juhudi darasani.
Ni mwishowe, yeye kati ya watoto sita ndiye pekee aliyefaulu kidato cha nne na kuendelea na masomo ya kidato cha tano kwani ndugu zake watano waliishia darasa la saba, kidato cha pili na waliofika kidato cha nne walifeli na kuozwa ili familia inufaike na mifugo na fedha za mahari.
"Famili yetu ina watoto sita, watatu wa kiume na idadi ya wasichana ni watatu pia, kaka zangu wameshaoa kwasababu walishindwa kusoma na wawili walifika kidato cha nne ila wafeli na mmoja aliishia la saba. Dada zangu waliishia kidato cha pili na kuozwa na mwingine aliacha masomo akiozwa ila sikutaka hili linitoke," anasema Kashinje.
Anakumbusha kuwa wakati akisubiri matokeo, mchumba wa kwanza alijitokeza kwa shinikizo la baba yake, aliyemtoza mahari ya ng'ombe 10 na Shilingi 300,000, alivyoshindwa kukidhi kiwango hicho aliondoka, hatua iliyomwongeza ari ya kuendelea na shule.
Kashinje anasema, wiki mbili baadaye alijitokeza wa pili baada ya kuzungumza na wazazi wakakubaliana alipe ng’ombe saba na Sh.200,000. Mama yake hakuwa na sauti hivyo alikubali aache masomo aolewe, lakini kipindi hicho matokeo yalitoka akapata ufaulu wa daraja la pili.
"Sikutaka kuolewa kabisa kwasababu nilitaka kusoma na nilikuwa nimefaulu kwenda kidato cha tano, familia nzima na majirani wanaonizunguka walinishawishi nikubali yaishe ila akili kichwani. Nilionekana binti wa Kisukuma asiye na heshima tena kwa kukataa matakwa ya wazazi wanaona kesho yangu,” anasema Kashinje.
Anamtaja mwalimu wake wa sekondari Boniphace Madurya, baada ya kupata taarifa hizo alikwenda kuripoti katika vyombo vya sheria na mama yake alikamatwa na kupelekwa polisi.
Anadai kituoni hapo walihonga Sh.500,000 na kutoka wakiwa na msimamo huohuo hadi Ofisi ya Ustawi wa Jamii ilipoingilia kati na kuzuia ndoa hiyo na kumpeleka kwa mjomba wake anayeishi Mipa Kishapu, mwenye uelewa wa masuala ya elimu.
Anasema kutoka nyumbani kwake alikwenda kusoma kidato cha tano na sita na mwaka 2022 alipohitimu alirejea nyumbani, akipokelewa na sasa yuko Chuo Kikuu SUA.
Anasema shahada anayosoma ni ya maendeleo ya jamii akitarajia kuwa balozi wa kukabiliana na ndoa za utotoni.
SAUTI YA MAMA MZAZI
Theresia Bupamba ni mama mzazi wa binti huyo, anakiri walitaka kumwozesha mtoto wao ili kuisaidia familia kuondokana na umasikini.
“Kama unavyojua utajiri wa Wasukuma ni mifugo hasa ng'ombe hivyo nilitakiwa kumshawishi mwananangu akubali kuachana na shule akaolewe,” anasema Theresia.
Anaongeza kuwa awali alikuwa akishirikiana na mwanawe kupinga kuozwa kwani ndugu zake walishindwa masomo na kuozwa ndio sababu mchumba wa kwanza alipofika walimtajia mahari kubwa ya ng'ombe 10 na Sh.300,000 ili aondoke ili kumpa nafasi binti yake kusoma kwani alifaulu vizuri.
"Niliposikia amepelekwa kwa mjomba wake hofu yangu ilitoweka nikajua atasoma na kutimiza ndoto zake na ameonyesha ujasiri wa kujisimamia na kuhakikisha haolewi na sasa kiu yake ya kufika chuo kikuu na kusoma kile anachohitaji imetimizwa," anaongeza Theresia.
MABINTI WANAUMIZWA
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Msalala, Richard Ng'ondya, anasema, ukatili kwenye jamii umeshamiri kwa kiwango kikubwa na mabinti wanakosa masomo.
Aidha kwa kushawishiwa na wazazi wasifanye vema kwenye mitihani ya mwisho ili wafeli na kuozwa na wengine kutoroshwa na kutolewa masomoni.
Anasema, binti Kashinje alionyesha ujasiri wa kupambana asiolewe na kuhakikisha anatimiza ndoto zake za kufika chuo kikuu ndio sababu walipopata taarifa za tukio hilo walifika mara moja na kumhifadhi sehemu salama kabla ya kumpeleka kwa mjomba wake huku wakiendelea kuchukua hatua kwa wazazi wake.
Ng'ondya anasema, wazazi wake walipatia elimu ya ukatili wa kijinsia na kwa kuwaeleza kile walichokuwa wanakifanya ni kosa na watakiwa kushtakiwa na kukubali kutoa ushirikiano na kuchangia Sh.700,000 za maandalizi ya kidato cha tano na sita na wakati huo tayari binti yao alikuwa ameshapelekwa kwa mjomba Kishapu.
"Binti huyu ni jasiri na anapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwenye jamii, alijisimamia asiozwe na sasa yuko chuo kikuu, tulipopata taarifa zake tulimhifadhi kwa ofisa maendeleo wa kata yake kwa muda na baadae mimi mwenyewe nilimbeba mpaka kwa mjomba wake anayeishi Mipa-Kishapu na alitokea hapo kwenda Shule Korogwe-Tanga"Anasema Ng'ondya.
Aidha anasema, kwasasa wana kituo cha huduma ya shufaa kipo kata ya Bugarama na kina daktari, dawati la jinsia na ustawi wa jamii na kwa siku wanapokea mashauri manne hadi sita na kuwataka wananchi kukitumia katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyotokea ili kuvidhibiti.
WAPAZA SAUTI
Mwenyekiti wa Wanawake 100,000 Taifa, Anascolastika Ndagiwe, anampongeza binti huyo kwa kuonyesha ujasiri wa kukataa kuozwa, licha ya wazazi wake wanaomzunguka kumkatisha tamaa ya kuwa sio vema kukataa kuolewa na mahari kurejeshwa kwa madai ni kujitafutia mikosa kwenye maisha jambo ambalo si kweli.
Anasema, wazazi wanatakiwa kuwajibishwa kisheria kwa walilotaka kulifanya ili iwe fundisho kwa wengine wenye tamaa ya mali wanaokatisha ndoto za mabinti zao, akiziomba mamlaka zilizomsaidia binti huyo kufuatilia ndugu zake walioozwa kama waliolewa wakiwa na umri sahihi.
Sheria ya Mtoto ya 2009 sura ya 13, kifungu cha nane kifungu kidogo cha pili inawaonya wote wanaomnyang’anya mtoto haki ya kupata elimu, chakula, mavazi, malazi, huduma za afya au kitu chochote kinachohitajika kwa ajili ya maendeleo yake.
Hata hivyo Sheria ya Ndoa 1971 imekuwa na kigugumizi katika kudhibiti ndoa za utotoni na kuzidi kuwapa kiburi wazazi wanaoendekeza vitendo hivyo. Sheria hiyo imewataja wafunga ndoa kuwa ni wale waliotimiza umri wa miaka 18.
Huku ikibainisha kuwa chini ya umri huo iwapo tu kibali kimetolewa na wazazi kwa binti aliye chini ya miaka 15 na mahakama kwa aliye chini ya miaka 14.
Mwanaume anaweza kuruhusiwa na mahakama kuoa akiwa chini ya miaka 18 lakini si chini ya miaka 14 kama ataonyesha kuelewa jukumu lake kama mtu mzima.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED