ILIKUWA Mei mwaka jana, mapacha Kulwa na Dotto Mahenga, wakazi wa kijiji cha Lyandu katika Manispaa ya Shinyanga, wakiwa kwenye pikipiki, walipata ajali kwa kugongwa na gari na kufariki dunia papo hapo.
Vifo hivyo vilitokea kwenye barabara iendayo Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga, ambayo imekuwa ikilalamikiwa kutokana na ubovu wake, tangu kuanza kutolewa huduma katika hospitali hiyo mwaka 2022.
Mzazi wa watoto hao, Zainab Tagala, anasema kifo cha watoto wake ni pigo kubwa kwake na familia, kwani pia alikuwa akiwategemea kuendesha maisha yake, baada ya baba yao kufariki dunia, huku kaka yao mkubwa anajitegemea na familia yake.
Mama Zainab, anaeleza: “Barabara ya hospitali isingekuwa mbovu, watoto wangu sasa hivi wangekuwa wazima, yaani nikifikiria naanza kulia.”
Anaendelea kwa majonzi: “Na siwezi kuzungumza tena!... Nenda ukaongee na kaka yao kwenye mji wake upo jirani tu na hapa, nasikia uchungu sana.”
Nipashe inapolazimika kubadili mwelekeo, hadi kwa kaka wa vijana hao, Mohamed Shabani, anasimulia walipokea taarifa ya ajali ya wadogo zake, Kulwa na Dotto kwa mshtuko mkubwa.
Anasimulia, kwamba waligongwa wakati gari lilipokuwa ikikwepa mashimo katika barabara hiyo ya Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga.
Shabani anasema, aliwaacha wadogo zake nyumbani kama nguzo ya familia na baada ya vifo hivyo “wamelia na wamenyamaza” na kuomba serikali iiangalie barabara hiyo kwa jicho la tatu.
Maoni yake ni kwamba, mahali hapo panapitiwa na watu wengi na imekuwa ikikatwa na maji pale mvua zinaponyesha.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Luzila John, kila siku moja huwa wanahudumia wagonjwa zaidi ya 200.
Mwongozo wa ujenzi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga wa Mwaka 2014, unaonyesha michoro ya majengo, ikiendana na kuwapo na ubora wa barabara.
Dk. Luzila anasema, hospitali hiyo ilianza rasmi kutoa huduma za matibabu mnamo Desemba 29, 2022, hivyo hadi sasa ina miezi 24 au miaka miwili na wiki mbili.
Anasema, kutokana na uhitaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi wa mkoa huo, ilibidi waanze kutoa huduma hivyo, licha ya ubovu huo wa barabara ulipo.
Dk. Ruzila anasema kwamba, ubovu wa barabara hiyo kutojengwa kwa muda mrefu, binafsi amekuwa akiwasilisha malalamiko yake mara nyingi, kwenye vikao mbalimbali vya viongozi.
Anataja baadhi yake ni pamoja na Kamati ya Ushauri cha Mkoa huo (RCC), akirejea kikao cha Desemba 15 mwaka 2023, lakini hakuna utekelezaji wake.
Kwa mujibu wa Dk. Ruzila, ubovu huo wa barabara, umekuwa ukisababisha vifo na kuhatarisha maisha ya wagonjwa, na kwamba magari ya wagonjwa.
“Ambulance (magari ya wagonjwa) zimekuwa zikipata ajali, huku zikiwa zimebeba wagonjwa, jambo ambalo ni hatari...
“Athari za ubovu wa barabara hii ni kubwa! Mfano ukiwa umembeba mgonjwa aliyevunjika mifupa au mjamzito, hadi kufika hospitalini hapa, atakuwa amepata maumivu makali sana na kuhatarisha afya yake,” anaeleza.
Kwa mujibu wa Dk. Luzila, pia magari ya hospitali hiyo yamekuwa yakiharibika na kuingia gharama za matengenezo ya mara kwa mara na kwamba gari moja hadi sasa wamelipaki baada ya kukosa fedha za kulitengeneza.
GARI LA WAGONJWA
Dereva wa gari la kubeba wagonjwa (ambulance) katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga, John Mabelele, anataja changamoto wanazopata kutokana na ubovu wa barabara ya hospitali hiyo.
Anataja baadhi ya athari ni kuuharibika magari yao, ajali na kwamba wakuwa wakiwabeba wagonjwa wenye hali mbaya, wanailalamika kuumia.
Anafafanua kuwa, pia mvua zinaponyesha, barabara hizo zinakuwa mbaya zaidi, kwa sababu mashimo yake yanafukiwa na maji, hivyo inakuwa ngumu kwao madereva kuyaona na wanajikuta wakivunja ‘shock up’ za magari, huku wakiwaumiza wagonjwa.
WATUMIA BARABARA
Safari ya kupata ufafanuzi za Nipashe, ziliifkisha kwa mgonjwa Letecia Dotto, anayeeleza uzoefu wake, akisema wanaposafiri kwa bajaji kupata matibabu hospitalini hapo, akiwa amebebwa kwenye bajaji, alikuwa akisikia maumivu makali, hasa kunapotokea mtikisiko.
Anaungana na mtumiaji barabara, Kuluthumu Mohamed, anayesema magari yao yamekuwa yakiharibika kila mara na haipiti wiki, lazima waende kufanya matengenezo, yakiwagharimu kiasi kikubwa cha fedha.
KAULI YA RPC
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi, anaungana na kauli zilizotangulia za adha ya Barabara hiyo kuwa vyanzo vya ajali nyingi katika Manispaa Shinyanga.
“Siwezi kuchambua kwamba katika barabara hiyo zimetokea ajali ngapi, matukio haya tunajumlisha kwa ujumla,” anasema TPC Magomi.
Mratibu wa ujenzi wa miundombinu ya Afya Mkoa wa Shinyanga, Faustine Mlyutu, anasema maeneo yote ya kutoa huduma za afya na kisera yanapaswa yawe na miundombinu rafiki ya wagonjwa kufika kwa urahisi penye matibabu, pasipo vikwazo.
“Kitu ambacho huwa tunakizingatia kwenye ujenzi wa huduma za afya, ni kuhakikisha miundombinu ya usafiri inakuwa rafiki kwa wagonjwa na kunapotokea changamoto huwa tunawasiliana na TARURA kufanya matengenezo ya barabara,” anasema Mlyutu.
TARURA & MABOSI MKOANI
Meneja Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) wilayani Shinyanga, Mhandisi Samson Pamphili, anasema walishapokea maombi ya ujenzi wa barabara hiyo kutoka kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa.
Anataja tatizo linalokwamisha ujenzi wa barabara ni ufinyu wa bajeti, ila kwa sasa wamepata fedha kutoka ufadhili wa Benki ya Dunia shilingi bilioni tisa za kujenga barabara mbili, daraja na miundombinu itakayosaidia kufika hospitalini kirahisi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, anakiri ubovu wa barabara hiyo ni tatizo kubwa kwa wagonjwa kufika kupata huduma katika hospitali ya mkoa huo.
Anasema, kwa sasa barabara hiyo imeingizwa kwenye mpango wa Benki ya Dunia na ujenzi wake unatarajiwa kuanza mwezi Februari au Machi mwaka huu.
“Barabara hii ya kwenda Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga ni mbovu sana na wananchi wamekuwa wakiipigia kelele na kipindi cha kiangazi huwa kuna vumbi,” anasema Macha.
Anahitimisha kwamba “inapofika Msomu wa Masika, utelezi ni mkubwa na ina mashimo, lakini serikali ipo katika hatua nzuri ya kuijenga.”
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Watu wenye ulemavu, anasema barabara hiyo ilikwama kujengwa sababu ya mifumo ya kifedha.
Anaungana kwamba, kwa sasa wanasubiri pesa kutoka Benki ya Dunia, ili waanze kutekekeza mradui wa Barabara inayofika hospitalini.
MWONGOZO KITAIFA
Hayo yanayotokea, huku Sera ya Afya ya Mwaka 2007, kifungu cha 5 (b) kinazungumzia “huduma bora za afya zinazowafikia wananchi wote kwa urahisi,” ambayo kipekee inabeba msisitizo wa kuwapo barabara bora, ‘pafikike kirahisi.’
Vilevile, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, Juni 13 mwaka huu bungeni Jijini Dodoma, katika hotuba yake ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025, akataja takwimu; watu 7,639 wamepoteza maisha kwa ajali za barabarani kwa miaka mitano; 2019-2024, pia majeruhi 12,663.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED