KWENYE tasnia ya muziki wa dansi, hasa wa zamani kuna hadithi nyingi sana zinazozungumzwa, zilizozungumzwa, lakini pia kuna zile ambazo hazijazungumzwa pia.
Pamoja na mashabiki wa muziki wa dansi hasa ule wa miaka ya kuanzia 1960 hadi mwishoni mwa miaka ya 1990 kusikiliza na kufurahia muziki huo, bado kuna mambo mengi ambayo yamepitika na bado watu hawakuyajua.
Kwa sasa angalau mashabiki wamekuwa wakisikia maelezo mengi, kama vile muziki fulani ulipigwa kwa madhumuni gani, lakini inavyoonekana muziki huo bado una hadithi nyingi ambazo zitaendelea kuibuka vizazi kwa vizazi.
Labda wakati huo watu walikuwa hawajui kwa sababu hakukuwa na vyombo vingi vya habari na mitandao ya kijamii.
Kukosekana kwa wachambuzi siku za nyuma ambayo wangekuwa na uwezo wa kudodosa hili na lile, nalo liliwanyima nafasi mashabiki kujua vitu vingi.
Kwa sasa kuna habari na hadithi nyingi zinajitokeza na kuzungumza hadi mtu unashangaa.
Mfano, bendi ya Bana Ngenge ambayo ilitisha sana miaka ya 1980 nchini Kenya, kumbe ilikuwa nchini Tanzania na kulazimika kukimbilia nchini humo kwa kuikimbia Orchestra Safari Sound chini ya mtindo wa 'Masantula Ngoma ya Mpwita' ikiongozwa na King Kiki.
Mmoja wa wanamuziki wa (OSS) hivi karibuni alikaririwa kwenye vyombo vya habari kuwa awali Bana Ngenge ndiyo ilikuwa ikipiga Safari Resorts. Lakini walipokuja wao awali walidharaulika, lakini baadaye Bana Ngenge aliona moto ni mkali wakakimbia nchi.
Si wengi wanaojua kuwa kumbe Ndala Kasheba alikuwamo kwenye kikosi cha OSS Masantula Ngoma ya Mpwita ya Kiki kama mwanamuziki wa kawaida, akiwa na mkwe wakati huo, Bakambi Nkela ambaye naye alikuwa mwimbaji.
Wengi wanajua kuwa Kiki alipoondoka ndiyo akaja Kasheba. Ukweli ni kwamba awali Kasheba alikuwepo kwenye kikosi cha kwanza, lakini kabla ya kurekodi akaondoka yeye na mkewe kwenda nchini Burundi kimuziki.
Baada ya mkataba wa Kiki na OSS kumalizika, ndipo mmiliki wa bendi hiyo, Hugho Kisima alipomrudisha Kasheba ambaye aliasisi mtindo wa Dukuduku.
Nadhani si mashabiki wengi pia wanaofahamu kuwa mwimbaji Lovy Longomba aliyewika nchini Kenya na Super Mazembe akaja nchini kujiunga na bendi ya African Sound 'Afriso Ngoma', ameshawahi kuimbia Maquiz Original na Bicco Stars kwa vipindi vifupi.
Kabla ya kuingia Afriso alikuwa Maquiz, lakini alidakwa na mmiliki wa bendi hayati Juma Mwendapole na kumpeleka kwenye bendi yake.
Kabla ya kuunda bendi yake ya Super Lovy alipotoka Afriso, mwanamuziki huyo mwenye sauti nyororo alijiunga Bicco Stars alifuata rafiki yake Ramadhani kinguti kwenye sauti nzito na alikuwa naye Afriso. Wengi hawajui habari hizo kwa sababu huko alikopitia hakurekodi.
Hata mpiga solo marehemu Mosesengo Fanfan ambaye wengi nchini wanajua alizipigia bendi ya Super Matimila na Orchestra Makassy, aliwahi kujiunga na Maquiz Original, lakini aliondoka kabla ya kurekodi, ndiyo maana wengi hawajui.
Leo nawapa hadithi ya bendi kongwe ya Dar Jazz ilivyotaka kupinduliwa na bendi yake ya kikosi cha pili.
Zamani bendi nyingi zilikuwa na vikosi vya pili kama timu za mpira wa miguu. Kikosi cha pili cha Dar Jazz kilipata mwanamuziki Patrick Balisidya. Hakuweza kuwemo kwenye kikosi cha kwanza kwa sababu kulikuwa na mkongwe King Michael Enock ambaye alikuwa akipiga solo.
Balisidya alipiga solo na kuimba. Ilikuwa mwishoni mwa miaka ya 1960, Dar Jazz ilikuwa ikifanya onyesho kwenye kumbi moja Dar es Salaam. Cha ajabu watu walikuwa ni wachache na si kawaida.
Muda mfupi baadaye ikaja taarifa kuwa mashabiki wengi wa Dar Jazz wamefurika kwenye onyesho la Dar Jazz B. Hiyo ilimshtua King na mmiliki wa kundi hilo.
Kumbe Balisidya alipopelekwa kwenye kikosi cha pili, alitumia kipaji chake cha kupiga solo na kuimbaji kukibadilisha kikosi hicho na kuwa tishio si kwa Dar Jazz pekee, bali hata baadhi ya bendi zingine.
King akamwambia mmiliki kuwa bila kuua bendi hiyo, Dar Jazz kubwa itapata shida sana kwa sababu mashabiki wameshatokea kuikubali na kupenda muziki wake.
Ni kwa sababu bendi hiyo ilipiga miziki yenye staili zote za kisasa na kizamani. Ilipiga miziki ya kizungu kama ile ya kina James Brown, Kikongomani, mtindo kama ya Dar Jazz yenyewe kubwa, halafu wakatunga na kuimba nyimbo zao kisasa zaidi, hivyo kufanya mashabiki kuanza kuikacha bendi kubwa.
Mmiliki akavunja kikosi cha pili cha Dar Jazz. Wale wanamuziki walioonekana wakali, kama Balisidya na wengine wachache wakapandishwa kwenye kikosi cha kwanza.
Hii ilimuuma sana Balisidya kwani alishaanza kutengeneza kama utawala wake hivi na umaarufu.
Kwa jinsi alivyoteka mashabiki, aliona ilikuwa ndiyo njia yake ya kutengeneza jina.
Hata hivyo ilimfunza kitu. Alijiona kumbe anaweza, hivyo lake lilikuwa rohoni.
Aliendelea kupiga Dar Jazz, lakini akiwa na sononeko moyoni hadi aliposaidia na baba yake mzazi kununua vyombo na kuunda bendi ya Afro Band, ambayo ilijulikana kama Afro 70 kutokana na kuundwa miaka hiyo na kujipatia umaarufu mkubwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED