Wizara ya Afya yatoa onyo wanaobandika kope bandia, kiini cha macho

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 06:32 PM Oct 30 2024
Mratibu huduma ya macho kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Rajab Muhamed Hilali

Mratibu huduma ya macho kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Rajab Muhamed Hilali amesema kuwa kuna ongezeko kubwa la wanawake wanaobandika kope bandia na kiini cha macho (lease) jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.

Akizungumza na Nipashe Digital Visiwani Zanzibar mtaalamu huyo amesema ni hatari kiafya kufanya urembo huo na kunauwezako wa kupoteza uoni au kuwa na uoni hafifu kutokana na urembo huo.

Amesema ongezeko hilo la watumiaji wa kope na 'lease' linatokana na masuala ya utandawazi bila ya kujali athari ya jicho hasa ikizingatiwa ubandikaji wa kope hutumia gundi maalum ambalo linatengenezwa kwa kemikali.

Amesema kuna kesi nyingi zimeripotiwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja na kutoa matibabu kwa watu waliopata athari ya ubandikaji wa kope bandia pamoja na 'lease' kiini cha jicho ikiwemo kupata vidonda katika jicho.

Aidha amewataka watumiaji wa kope kuchukua tahadhari kwa sababu unaweza kufanya kwa madhumuni ya urembo lakini baadae ikawaletea athari kubwa.