MASHIRIKA 500 yasiyokuwa ya kiserikali na washiriki zaidi ya 600 wa hapa nchini na nje ya nchi, watashiriki katika wiki ya Azaki itakayofanyika jijini Arusha, kuanzia Septemba 9 hadi 13 mwaka huu.
Hayo yalisema jana jijini hapa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Wiki ya Azaki mwaka 2024, Nesia Mahenge,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea ufunguzi wa wiki ya Azaki itakayofanyika kwa siku tano.
Alisema kuwa jumla ya washiriki zaidi ya 600 kutoka hapa nchini na nje ya nchi mashirika 500 yatashiriki kwenye mkutano huo wa Azaki.
Hata hivyo,alisema mgeni rasmi atakuwa ni Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo,pia kutakuwapo na viongozi wengine kutoka nje ya Tanzania akiwamo Balozi wa Umoja wa Ulaya(EU) na Balozi wa Canada.
Alisema lengo la mkutano huo, kwa mashirika hayo yasiyokuwa ya kiserikali ni kukutana na kujifunza,kubadilishana uzoefu kutoka kwenye mashirika hayo.
Alisema pia watakwenda kwenye jamii kuangalia mambo yaliyofanywa na Serikali katika jitihada za kuwaletea maendeleo wananchi na Watanzania kwa ujumla.
"Kama mashirika yasiyokuwa ya kiserikali tutaangalia namna ya kuwawezesha wananchi katika jitihada zilizofanywa na Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi wetu,"alisema.
Naye John Kalaghe, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la HakiElimu, alisema katika wiki hiyo ya Azaki,watakuwa na kipindi cha ushiri wa vijana hasa katika michakato ya kidemokrasia ndani na nje ya mifumo ya shule.
"Tumeandaa sesheni ya vijana ambayo watazungumza juu ya ushirika wao katika suala la michakato ya kidemokrasia,"alisema.
Licha ya kuzungumza hayo,alisema tofauti ya mijadala mingine,watawakutanisha vijana na watapata fursa ya kujadiliana kuhusu ushirika wao katika michakato hiyo.
"Lengo la kuandaa sesheni hii kwa vijana ni kuwahamasisha kushiriki katika michakato ya kidemokrasia kwa kuwa ukiangalia tafiti mbalimbali zilizofanyika ushirika wa vijana katika michakato hiyo ni hafifu.
"Tunataka kuangalia na kujadiliana umuhimu wa vijana kushiriki kwenye michakato hiyo, kwa kuwa mwaka huu na mwakana kuna fursa kwa kundi hili kuchukua fomu za kugombea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.alisema"
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Foundation for Civil Society(FCS),Justine Rutenge,alisema katika wiki hiyo ya Azaki kutakuwepo na mada mbalimbali ikiwamo ya suti,dira na thamani.
"Tuko katika kipindi ambacho kina michakato ya kidemokrasia kwa kuwa tunaelekea kwenye uchaguzi wa serikali mitaa, uchaguzi Mkuu wa mwakani na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, hivyo vijana watapata fursa ya kupaza sauti zao kwa kuwa ni muhimu kwao.
"Tutaweza kuangazia sauti hasa za pembeni katika michakato hiyo ya kidemokrasia ili sauti hizo zisikike.alisema"
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED